Qatar kushiriki katika uchimbaji wa gesi katika pwani ya Lebanon
Uchimbaji wa gesi kusini mwa Lebanon hatimaye utaanza hivi karibuni. Qatar iliingia, mnamo Jumapili Januari 29, kama TotalEnergies ya Ufaransa na ENI ya Italia katika muungano wenye dhamana ya kuendesha shughuli zake za uchimbaji gesi katika eneo hili la bahari kwenye mpaka na Israel.
Imechapishwa:
Qatar itashikilia 30% ya hisa katika muungano huu, dhidi ya 35% kwa TotalEnergies na 35% kwa ENI. Emirate ya Ghuba inachukua nafasi ya Novatek ya Urusi, ambayo ilijiondoa katika mradi huo mnamo 2022.
Ushiriki wa Qatar sio tu kwamba unatoa msaada wa kifedha kwa mradi huu, lakini zaidi ya yote unajumuisha dhamana ya kisiasa, hasa kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya Qatar na nchi za Magharibi na hata Israel, amebaini mtaalamu wa nishati Naji Abi Aad akihojiwa na shirika la habari la AFP.
Kwa hivyo uchunguzi unaweza kuanza katika uwanja unaowezekana wa Kana, ambao sehemu yake iko katika maji ya eneo la Israeli. Israel itapokea fidia ya kifedha kulingana na makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana na Lebanon baada ya upatanishi wa muda mrefu wa Marekani.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa TotalEnergies, mchakato wa uchimbaji unapaswa kukamilika kwa takriban mwaka mmoja. Ugunduzi unaowezekana wa gesi utakuwa pumzi ya matumaini kwa Lebanon iliyotumbukia katika mzozo wa kiuchumi ambao haujawahi kutokea. Lakini nchi hii italazimika kusubiri miaka kadhaa kabla ya uzinduzi wa uzalishaji.