Pata taarifa kuu
NDONDI

Mashindano ya Nairobi Fight Night yatazamiwa 'kuinua' ndondi ya Afrika Mashariki

Nairobi – Mashindano ya Nairobi Fight Night, yatainua mchezo wa ndondi Afrika Mashariki kwa kasi ya juu ili kufikia viwango vya ndondi ya kimataifa, kulingana na mwakilishi wa WBF barani Afrika, George Adipo.

Bondia wa Tanzania Meshack Mwankemwa (kushoto) na Rayton Okwiri wa Kenya (kulia) wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea pambano lao la uzito wa kati la World Boxing Foundation Machi, 23 2024 ukumbini KICC, Nairobi.
Bondia wa Tanzania Meshack Mwankemwa (kushoto) na Rayton Okwiri wa Kenya (kulia) wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea pambano lao la uzito wa kati la World Boxing Foundation Machi, 23 2024 ukumbini KICC, Nairobi. © KPBC
Matangazo ya kibiashara

Kampuni ya Solid Rock Promotion kwa ushirikiano na AiWEx Sports na Shirikisho la mchezo wa ndondi nchini Kenya (KPBC) wiki hii ilizindua msimu mpya wa mashindano ya ndondi ya Nairobi Fight Night.

“Ni kitambo sana mkanda kama huu kuchezewa hapa Kenya. Vijana wadogo wakiona huu mkanda itawapa motisha ya kung’ang’ania mikanda kubwa kubwa,” alisema George Adipo.

“Tanzania wako mbele kidogo sababu wana mabondia wengi, runinga ya Azam na wadhamini wengi inawasaidia sana. Tunaomba wadhamini wajitokeze kwa wingi.”

Msimu wa mwaka 2024 utashuhudia mashindano matano yakiandaliwa kwa wakati tofauti. Shindano la kwanza litaandaliwa tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi nchini Kenya. Mkurugenzi wa AiWex Sports, Willy Wex katika sherehe ya uzinduzi jijini Nairobi, aliahidi mashabiki msimu wa kukata na shoka kwenye mashindano yatakayofuata ya tarehe moja Juni, Agosti 10, Oktoba 20 hadi Disemba 14.

Maandalizi yanazidi kupamba moto kuelekea pambano la raundi 10 la uzito wa kati la World Boxing Foundation (WBF) kati ya Rayton Okwiri wa Kenya na Meshack Mwankemwa wa Tanzania tarehe 23 Machi.

Okwiri, Mwankemwa na viongozi wa pigano la Nairobi Fight Night
Okwiri, Mwankemwa na viongozi wa pigano la Nairobi Fight Night © Jason Sagini

Okwiri ambaye ameshiriki mashindano ya Olimpiki na ni mshindi mara nne wa taji la bara Afrika (ABU) alimuonya Mwankemwa kujiandaa kwa pambano hilo gumu. Alisema Mtanzania huyo atakuwa na bahati endapo atavuka raundi ya kwanza.

“Kwanza nimpongeze Mwankemwa kwa kuonyesha uhodari wake na kukubali ombi la kupigana nami. Hata hivyo, anapaswa kuwa tayari kupigwa.”

"Nimejiandaa vya kutosha, nilipaswa kupigana Mauritius mwezi uliopita lakini iliahirishwa. Hiyo ina maana niko tayari zaidi kwa pambano hili, nitacheza kimbinu. Atakuwa na bahati ya kumaliza raundi ya kwanza," alisisitiza Okiri kwa kujiamini.”

“Nina uzoefu kumshinda Mwankemwa.”

Aliendelea kusema: "Lengo langu ni kuwa bingwa wa dunia kabla sijasherehekea siku yangu ya kuzaliwa ya 40, hivyo pambano hili linanipa nafasi nzuri ya kutimiza ndoto yangu."

Tazama majibizano kati ya Rayton Okwiri na Meshack Mwankemwa

Mwankemwa hakusita kujibu cheche za Okwiri.

"Nimewashinda mabondia wazoefu kama Okwiri hapo awali, sina wasiwasi naye hata kidogo. Ikiwa nilifanya vyema dhidi ya mabondia wakubwa kutoka Ulaya, Urusi na Kazakhstan, Okwiri ni nani wa kunizuia? Tuko Kenya kwa misheni,” alisema Mwankemwa.

“Mimi mwenyewe nishakuwa bingwa sana, ubingwa kila mtu ni bingwa, ngumi itakuwa nzuri.”

Kocha wake Mwankemwa, Benson Nyirawira alisema Meshack Mwankemwa ni ‘malaika mtoa roho’ na wamekuja nchini Kenya “kumtoa roho Rayton Okwiri.”

“Maisha ya Okwiri ya sasa yako mikononi mwa Mwankemwa, tutampiga kipigo kitakatifu,” alisema kwa ujasiri kocha Benson.

Rais wa ndondi nchini Kenya, Reuben Ndolo pia alisema wanatazamia pambano la kiwango cha juu kati ya wapinzani hao wawili.

Mwakilishi wa WBF barani Afrika, George Adipo akishikilia mkanda wa WBF intercontinental utakaopiganiwa kati ya Okwiri na Mwankemwa
Mwakilishi wa WBF barani Afrika, George Adipo akishikilia mkanda wa WBF intercontinental utakaopiganiwa kati ya Okwiri na Mwankemwa © Jason Sagini

Mshindi wa pigano hilo atafuzu moja kwa moja kupambania mkanda wa dunia wa WBF. Pigano hili aidha litashuhudia mechi zingine 11 kuchezwa kabla yake.

Aidha promota au mwakilishi wa Solid Rock Promotion Mike Odongo aliahidi ukubwa wa pambano la kwanza akifichua mabondia kutoka Ufaransa, Canada, Uingereza, Uganda na Mauritius kuwasili nchini wiki moja kabla ya pigano ili kushiriki.

Promota huyo aliwataka wadhamini kujitokeza na kuwasaidia kufanya mashindano matano waliyopanga mwaka huu kuwa ya kufana.

"Hili ni taji la dunia na litaendelea hadi Desemba, tunawaomba wadhamini na washirika kujitokeza kutusaidia kuhakikisha tunaandaa tukio lenye mafanikio," alisema rais wa ndondi nchini Kenya, Reuben Ndolo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.