Pata taarifa kuu
Magical Kenya Open 2024

Ronald Rugumayo kutoka Uganda aweka historia kubwa mashindano ya DP World Tour

Muthaiga Gof Club, Nairobi - Kenya – Raia wa Uganda Ronald Rugumayo mwenye umri wa miaka 31 aliweka historia ya kuwa mganda wa kwanza kuwahi kupenya mchujo wa mashindano yoyote ya gofu kwenye msururu wa mashindano ya gofu duniani, baada ya kumaliza kwa alama ya PAR siku ya Ijumaa kwenye mashindano ya Magical Kenya Open 2024 yanayoendelea katika uwanja wa Muthaiga, jijini Nairobi nchini Kenya.

Ronald Rugumayo akianzisha mapigo kwenye shimo la tatu (Par4/3) uwanjani Muthaiga jijini Nairobi mnamo 23/02/2024
Ronald Rugumayo akianzisha mapigo kwenye shimo la tatu (Par4/3) uwanjani Muthaiga jijini Nairobi mnamo 23/02/2024 © DP World Tour
Matangazo ya kibiashara

Ronald alifunga birdie kwenye shimo la 18 na kumwezesha kumaliza siku ya pili ya mashindano kwa kusawazisha jumla ya mapigo 142 baada ya kumaliza pigo moja zaidi ya 71 (I over PAR 71) kwenye siku ya kwanza.

Pigo la kuingiza mpira shimoni haikuwa rahisi kwa umbali wa karibu futi kumi na karibia kushoto kwenye mlima mdogo uwanjani ilihitaji hukumu makini chini ya mteremko.

Robo tatu mbele, ilionekana kwamba pigo hilo lingekosa upande wa juu lakini Rugumayo alipochutama akiwa na matumaini zaidi ya matarajio, mpira wake uliingia kwenye ukingo wa kulia wa shimo.

Matokeo yake yalizalisha kishindo cha kuziba masikio kutoka kwa wale waliokuwa wakitazama. Hii ilimaanisha kitu, sio tu kwa mchezaji huyo.

"Kilichofanyika nilijua kitafanyika. Nimewekeza muda mwingi, kujituma zaidi. Nilistahili kufuzu," alisema Ronald akitabasamu.

"Ndio nimefuzu lakini ningali kufikia malengo yangu."

Kwenye siku ya pili, Ronald alirekodi birdie nne kwenye mashimo ya (par 5/4, par 4/9, par 4/15 na par 5/18) na bogey tatu kwenye mashimo ya (par 4/1, par 3/5 na par 5/7) ili kumaliza nafasi ya 65.

"Mashindano haya ni zaidi ya kupenya mchujo," alisisitiza Rugumayo ambaye anashiriki mashindano yake ya MKO kwa mata ya tatu.

Baada ya siku ya kwanza, Ronaldo alisema hayo (1 Over PAR71) yalikuwa matokeo yake bora zaidi kuwahi kupata kwenye siku ya kwanza ya mashindano ya MKO tangu kushiriki mara ya kwanza mwaka 2018.

Ronald Rugumayo baada ya kufunga birdie kwenye shimo la 18 kwenye Magical Kenya Open 2024
Ronald Rugumayo baada ya kufunga birdie kwenye shimo la 18 kwenye Magical Kenya Open 2024 © DP World Tour

Akiwa amefuzu kitengo cha washindi wa pesa wikendi hii, Ronald anasema atazidi kufukuzia malengo yake.

"Ningependa kumaliza nafasi nzuri tu lakini itategemea pakubwa nitakavyocheza."

"Sioni kikubwa cha kubadilisha. Kama mbinu nilizotumia zimeniwezesha kufuzu basi nitaendelea hivyo hivyo," aliainisha Ronald ambaye anaorodheshwa nafasi ya 2,901 katika msimamo wa gofu duniani.

Baada ya wakenya wote kukosa kufuzu mchujo, Ronald pia aliweka historia ya kuwa mzaliwa wa Afrika Mashariki pekee kusalia mashindanoni. Hili likiwavutia mashabiki wa nyumbani kumshangilia pakubwa kwenye hatua ya mwisho siku ya Ijumaa.

"Presha ya mashabiki ni kawaida. Ukiona kuna shinikizo basi ujue unacheza vizuri. Mimi napenda hali hiyo."

"Kiukweli, ukicheza bure tu hutahisi shinikizo, kila wakati ninapohisi presha huwa inanikumbusha nacheza kutafuta kitu kizuri,” alisisitiza Rugumayo.

Ijumaa ilikuwa kama usiku wa kiza kwa wachezaji wa nyumbani baada ya wote kukosa kupenya mchujo huo. Mkenya pekee kufuzu kwenye mashindano ya mwaka jana, Mutahi Kibugu alikuwa na mchana mrefu baada ya kuvuna mapigo sita zaidi ya 142 kwenye siku ya pili. Mutahi alifunga birdie moja na bogey mbili kwenye siku ya pili baada ya kufunga bogey sita, double bogey moja na birdie moja tu kwenye siku ya kwanza. Mshindi wa Safari Tour mwaka 2024 Dismas Indiza, 55, pia alikosa kufuzu kwa kurekodi matokeo ya mapigo mawili zaidi ya 142.

Ni matokeo ambayo baadhi ya wachezaji hawakusita kuonesha masikitiko yao.

“Kenya Open si mashindano rahisi ambayo utakuja tu na ushinde.Tunastahili kupewa fursa ya kushiriki mashindano mengi ya nje kabla ya haya ili tufanye vizuri,” alisema kwa sauti nyonge Dismas Indiza.

“Nimekosa kufuzu, bila shaka sharti nifanyie kazi kuboresha mchezo wangu,” alisema Samuel Njoroge.

Licha ya matokeo hayo, mchezaji wa Uskochi Ewen Ferguson na Dylan Fritteli walisifia viwango vya Mutahi Kibugu (23).

“Nilipendezwa na anavyopiga mpira na pia kwenye umaliziaji. Anahitaji uzoefu zaidi sababu anamiliki mbinu za kipekee,” alisema Fritteli.

“Ni kijana mchangamfu ana tabia nzuri uwanjani, namtakia mema siku zijazo,” aliainisha Ewen Ferguson.

Mishangao waliyopata wakenya pia iliwapata baadhi ya washindi wa zamani wa Magical Kenya Open, wakibanduliwa mashindanoni.

Mshindi wa mwaka 2019 Guido Migliozi alimaliza kwa jumla ya mapigo manne zaidi, mshindi wa 2021 Justin Harding – mapigo tisa zaidi ila mshindi wa 2022 Ashun Wu kutoka Uchina aliponea kwa kusawazisha PAR 142.

Tapio Pulkannen (Finland), Conor Syme (Scotland) na Darius van Driel (Uholanzi) wanaongoza jedwali kwa mapigo saba chini ya 142 kila mmoja.

Mshindi wa mashindano hayo atashinda dola milioni mbili nukta tano ($2,500,000) ambalo ni ongezeko la dola laki tatu kutoka kwa makala ya mwaka jana.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.