Pata taarifa kuu
AFCON 2023

AFCON 2027 inatabiriwa kuwa na 'mafanikio' kuliko Morocco 2025 na Ivory Coast 2023

NAIROBI – Kenya, Uganda na Tanzania hazitapata presha yoyote ya kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 baada ya Morocco kuandaa Afcon ya mwaka 2025, kulingana na Damas Daniel Ndumbaro, waziri wa utamaduni, sanaa na michezo nchini Tanzania.

Rais wa shirikisho la soka Afrika CAF, Patrice Motsepe akiidhinisha Kenya, Uganda na Tanzania kuwa wenyeji wa AFCON 2027, jijini Cairo Misri, Jumatano Septemba 27, 2023.
Rais wa shirikisho la soka Afrika CAF, Patrice Motsepe akiidhinisha Kenya, Uganda na Tanzania kuwa wenyeji wa AFCON 2027, jijini Cairo Misri, Jumatano Septemba 27, 2023. © https://www.cafonline.com
Matangazo ya kibiashara

“Wakati wa haya mashindano, watu wanapenda mpira na vitu vinavyoambatana na mpira ambavyo mara nyingi huwezi kuvipata Morocco kutokana na utamaduni wao wa kiarabu,” alisisitiza waziri Ndumbaro akiwa ziarani nchini Cote D’Ivoire kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2023.

“Sisi tutawapa vyote, tutawazidi Morocco kwa hilo.”

Waziri Ndumbaro alikuwa akizungumza nami kwenye mahojiano ya kipekee jijini San Pedro wakati wa mechi za Kundi F ambapo Tanzania ilikuwa mshiriki.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo pamoja na majirani wa Afrika Mashariki Kenya na Uganda - ikiwa ni mara ya kwanza katika historia kwa nchi tatu kuandaa mashindano hayo ya bara.

“Cote D’Ivoire kwenye mpira viwango vyao ni vya juu lakini kwenye maandalizi tumewazidi sana. Sisi tunaamini hata tukisema tufanye sasa tuko vizuri.”

Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo nchini Tanzania Damas Ndumbaro kwenye mahojiano na rfi kiswahili
Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo nchini Tanzania Damas Ndumbaro kwenye mahojiano na rfi kiswahili © Brown Kalaita

Caf haitashughulika na nchi mwenyeji mmoja mmoja bali kama chombo, na hivi karibuni mataifa hayo matatu yanatarajiwa kutaja kamati ya pamoja kuandaa.

Kando na kufuatilia timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ halikadhalika waziri Ndumbaro alizuru Ivory Coast “kuona wenzetu wamewezaje kuandaa miundo mbinu ya michezo – viwanja, hoteli, barabara – na kuandaa shindano lenyewe.”

Ni vipi Cote d’Ivoire iliweza kuwa na mpangilio mzuri wa mechi, afya na usalama kwa wachezaji, VISA, mipangilio ya usafiri kwa timu na kushirikisha sekta binfasi?

“Mji wa San Pedro ni mdogo sana,  ni sawa na Makambako huko kwetu Tanzania lakini umeweza kuandaa Afcon,” aliongeza.

Mojawapo ya vigezo vya CAF kuandaa AFCON ni mipangilio ya VISA – ambapo Damas anasema watakubaliana kuwa na VISA ya pamoja kusafiria kuenda Kenya, Uganda na Tanzania.

‘Changamoto za Kujifunzia’

Mechi kadhaa nchini Ivory Coast ikiwemo mechi ya ufunguzi ilikumbwa na changamoto katika kuuza tiketi. Rais wa CAF, Patrice Motsepe alikiri katika hotuba yake ya mwisho kwenye mashindano akidai “watu kadhaa walinunua tiketi zote kisha kuziuza kwa bei ya juu sana. Ndio maana hatukuona mashabiki wengi uwanjani.”

“Unapoona viti wazi uwanjani, si picha nzuri kwa soka la Afrika,” alisikitika Motsepe.

Waziri Ndumbaro anakariri suala hili kwa kudai waliambiwa tiketi za mechi ya Tanzania na Morocco zilikuwa zimeisha lakini baada ya kufuatilia wakagundua tatizo ni mfumo wa uuzaji wa tiketi.

Tiketi za mechi zilikuwa zinauzwa kwa kutumia mihamala ya simu tu kama njia pekee kando na kutumia pesa taslimu au kadi za benki.

Sherehe ya ufunguzi ya Afcon 2023 nchini Cote D'Ivoire
Sherehe ya ufunguzi ya Afcon 2023 nchini Cote D'Ivoire © CAF

“Sisi tunatakiwa kuanza kuziuza tiketi mtandaoni ikiwezekana miezi sita kabla na tunatakiwa turuhusu njia zote za kununa tiketi,” alisema Damas Ndumbaro.

Waziri Damas anaendelea kwa kudokeza kujifunza kutokana na hamasa ya mechi zote kando na za mwenyeji ambayo anasema ilikuwa changamoto nyingine kwa wenyeji Cote D’Ivoire kuhamasisha tu mechi zao na kupuuza mechi zingine.

Usafiri kuelekea uwanjani pia ulikuwa changamoto kubwa. Uwanja wa Olympic D’Ebimpe Alassane Ouattara umejengwa nje ya jiji la Abidjan na ni barabara moja tu ambayo inaunganisha jiji na uwanja huo. Ilinichukua takriban saa tatu na nusu kufika uwanjani siku ya ufunguzi, safari ambayo kwa kawaida ingenichukua saa moja.

“Tumejifunza kwamba njia zinazoelekea uwanjani lazima zitengenezwe vizuri, ziwe wazi na ziweze kupitisha magari mengi,” alikariri Damas.

“Lakini pia kuwe na maeneo ya kutosha ya kuegesha magari.”

“Ivory Coast wana uwanja mmoja wa ndege wa kimatafa, Afrika Mashariki tuna zaidi ya sita na pia wageni wanaweza kutumia usafiri wa maji.”

Hadhi ya viwanja 

Sehemu ya uwanja wa Laurent Pokou jijini San Pedro, Ivory Coast
Sehemu ya uwanja wa Laurent Pokou jijini San Pedro, Ivory Coast © Jason Sagini

Beijing & Constructors Group wajenzi wa uwanja wa Ouattara jijini Abidjan bado ndio wakandarasi wa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

“Wenzetu, kwenye ujenzi wa viwanja ulipewa kampuni tofauti na sehemu ya kuchezea (nyasi) ilipewa kampuni mahususi ambayo inashughulika na nyasi tu.”

“Umuhimu wa kubobea ni ubora wa matokeo.”

CAF itafanya ukaguzi wa viwanja na maandalizi ya AFCON27 mwezi Disemba mwaka 2025 – ina maana Afrika Mashariki ina miaka miwili tu kuwa tayari kuandaa mashindano hayo makubwa barani. Ujenzi wa viwanja vingine ambavyo vimeahidiwa kujengwa upya ungali kuanza huku pia ukarabati wa viwanja vilivyopo ukiendelea kwa mwendo wa kujikokota.

“Kwetu sisi huo muda unatosha, sehemu nyingi hatujengi viwanja vipya, tutaboresha vilivyopo,” alisisitiza Ndumbaro.

‘Mauzo ya Mashindano’

Mheshimiwa Ndumbaro anaamini Afrika Mashariki itauza mara tatu ya Ivory Coast kwa kutegemea mziki, chakula asili, utamaduni wa kiswahili na vivutio vya utalii.

“Tutauza sana kupitia utalii. Afrika Mashariki ina ‘Big Six’ si ‘Big Five’ ambayo watu huzungumzia – tuna gorilla (sokwe) ambaye anapatikana kwetu tu.”

Bwana Ndumbaro anamaliza mahojiano haya kwa kuahidi kufanya kikao cha pamoja na mawaziri wenzake (watakapofanya kikao na CAF cha kuandaa CHAN 2024) kuzuru viwanja vya Cote D’Ivoire tena ili kujifunza namna ya kujiandaa zaidi katika kuifanya Pamoja Afcon iwe nzuri na ya mafanikio makubwa.

“Tunataka tuweke alama kubwa Afrika ili wadau wa soka waseme hawakufanya kosa kuleta Afcon ukanda wetu.”

“Tunataka waseme hata yajayo yafanyike tena hapa.”

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.