Nigeria: Alex Iwobi akabiliwa na vitendo vya uonevu mtandaoni
Nairobi – Nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Nigeria Super Eagles amekuwa wa hivi punde kutoa wito wa kukomeshwa kwa vitendo vya uonevu mtandaoni dhidi ya kiungo Alex Iwobi.
Imechapishwa:
Mashabiki kadhaa wa soka wa Nigeria wamemtusi Iwobi kwenye mitandao ya kijamii, wakimlaumu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 baada ya nchi yao kufungwa 1-2 na Ivory Coast katika mchezo wa fainali ya Afcon siku ya Jumapili.
Iwobi alicheza kwenye mechi hiyo kwa dakika 79, kabla ya kundolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Alhassan Yusuf.
Iwobi amelazimika kufuta picha zake za Instagram siku ya Jumatatu baada ya kukabiliwa na uonevu huo kwenye mitandao ya kijamii.
Nahodha wa Super Eagles Ahmed Musa na baadhi ya raia wengine wa Nigeria wamemtetea Iwobi, wakilaani mashambulizi yaliyolengwa mtandaoni dhidi ya mchezaji huyo na kusema si haki kumtenga baada ya timu yao kupoteza.
Iwobi bado hajazungumza lolote kuhusu mashambulizi dhidi yake kwenye mitandao ya kijamii.