Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Je, CAF inapaswa kufutilia mbali fainali ya mshindi wa tatu kwenye AFCON?

Abidjan, Cote D'Ivoire – “Najivunia timu yangu kwa ushindi huu, lakini bado nitasisitiza tena mechi hii haistahili kuchezwa, nafasi ya tatu haimaanishi chochote, bado kuna kazi ya kufanywa,” alisema kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos baada ya Bafana Bafana kuishinda DR Congo katika uwanja wa Felix Houphouet Boigny, Abidjan kwenye mechi ya mshindi wa tatu.

Kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos kwenye mahojiano na wanahabari baada ya fainali ya mshindi wa tatu dhidi ya DR Congo
Kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos kwenye mahojiano na wanahabari baada ya fainali ya mshindi wa tatu dhidi ya DR Congo © CAF Media
Matangazo ya kibiashara

Katika Kombe la Dunia la 2014, kocha wa Uholanzi Louis van Gaal alikuwa na mawazo sawa na ya Hugo Broos kabla ya mchujo wa kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Brazil.

Nadhani mechi hii haipaswi kamwe kuchezwa. Nimekuwa nikisema hivi kwa miaka 10 iliyopita. Tutalazimika kucheza mchezo tu, lakini sio haki. Tutakuwa na siku moja tu ya kurejesha miili yetu sawa na huo sio mchezo wa haki. Jambo baya zaidi ni kwamba, ninaamini, kuna nafasi ya kupoteza mara mbili mfululizo kwenye mashindano ambayo umecheza vizuri sana. Unarudi nyumbani kama mshindwa kwa sababu labda umepoteza mechi mbili zilizopita.

Hivi kwanini AFCON inaendelea na utamaduni huu wa kizamani ambao hakuna anayeutaka?

Mechi ya mshindi wa tatu inahisi kama mchezo unaopendelea yeyote atakayepata nafuu baada ya kupoteza nusu fainali.

Kwenye makala ya mwaka 2021, wenyeji Cameroon walishindwa kufika fainali baada ya kupoteza nusu fainali dhidi ya Misri mabao 3-1 kwenye penalti kufuatia sare ya kutofungana.

Wachezaji wa Cameroon baada ya kupoteza mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Misri mwaka 2021.
Wachezaji wa Cameroon baada ya kupoteza mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Misri mwaka 2021. © FECAFOOT

Kocha wa Cameroon, Toni Conceicao aliwakusanya simba wake waliokatishwa tamaa, na kuwapa motisha kwa msukumo wa mwisho dhidi ya Burkina Faso katika mechi ambayo hakuna aliyetaka.

"Shinda kwa ajili ya watu!" alisihi, akijaribu kuingiza maana katika kile ambacho kimsingi ilikuwa ni mechi isiyo na maana.

Mshambuliaji, Vincent Aboubakar katika umri wa miaka 30, alijua ndoto yake ya kushinda AFCON labda haitotimia tena.

"Kwa nini tunawekwa katika hali hii,” Aboubakar alionyesha ghadhabu kwa wenzake.

“Mechi ya mshindi wa tatu haiamui chochote. Mashindano yetu yalimalizika jana usiku kwa jinsi ninavyohusika." Mwenzake alikubali kwa kutikisa kichwa tu.

Kocha wa Burkina Faso, Kamou Malo pia alilazimika kuwapa motisha vijana wake ili kuwania nafasi ya tatu.

“Ni mchezo wa kipuuzi,” alifoka Malo.

"Lakini lazima tubaki na kiburi chetu kwa Burkina Faso.”

Kwa kweli, wachezaji wake wangependelea kujihurumia kuliko kujihusisha na mchezo usio na maana.

Ni mechi ambayo katika uwanja wa mashabiki takriban elfu sitini, mashabiki chini ya elfu kumi na tano walihudhuria fainali hiyo.

Ni hali sawa na iliyoshuhudiwa jana uwanjani Boigny (uwanja wenye idadi ya watu 40,000) ambapo mashabiki 21,975 walihudhuria fainali ya mshindi wa tatu kati ya Afrika Kusini na DR Congo.

Sehemu ya mashabiki wa Afrika Kusini uwanjani Felix Houphouet Boigny katika mechi dhidi ya DR Congo mnamo 10/02/2024
Sehemu ya mashabiki wa Afrika Kusini uwanjani Felix Houphouet Boigny katika mechi dhidi ya DR Congo mnamo 10/02/2024 © Pierre René-Worms

Bafana Bafana mabingwa wa mwaka 1996, waliwacharaza DRC (mabingwa mara mbili 1968, 1974) mabao 6-5 kwenye mikwaju ya penalty kufuatia sare ya kutofungana muda wa kawaida bila muda wa ziada.

Baada ya Afrika Kusini kuwashinda DRC, kutokuwepo kwa hisia kali kulisema yote. Baada ya dakika chache za kusherehekea mlinda lango Ronwen Williams, shujaa wa penalti, mbwembwe hizo zilitulia.

Hakukuwa na medali yoyote, hakukuwa na jukwaa ila tu kupeana mkono kwa haraka kabla ya timu zote mbili kutoweka chini ya mtaro, sauti ya wimbo wa Akwaba wa Majic System ilitoa mwangwi karibu na uwanja usio na kitu.

Wachezaji wa Afrika Kusini wakimbeba juu kocha mkuu Hugo Broos baada ya kushinda mechi kwenye penalti
Wachezaji wa Afrika Kusini wakimbeba juu kocha mkuu Hugo Broos baada ya kushinda mechi kwenye penalti © Pierre René-Worms

Kuna maana gani kumtafuta mshindi wa tatu wakati nafasi ya tatu na nne kila mmoja atapokea dola milioni mbili nukta tano?

"Cha muhimu katika mashindano kama haya ni mshindi. Ukiwa wa tatu au wa nne, kwangu haina tofauti kwa sababu hii ni kwa ajili ya takwimu tu."

"Nambari ya kwanza ni muhimu, nambari moja itakumbukwa kila wakati," kocha Hugo Broos wa Bafana Bafana mwenye umri wa miaka 71 alisema siku ya Ijumaa, kabla ya fainali hiyo kuchezwa.

Kwa maana moja au nyingine, mechi hii ina haiba ya mechi ya kirafiki. Kocha wa DRC, Sebastian Desabre na mwenzake wa Afrika Kusini Hugo Broos walifanya mabadiliko mengi sana kwenye vikosi vyao ili kuwapa wachezaji wote nafasi ya kuonja ladha ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Kocha wa DRC, Sebastian Desabre baada ya kupoteza dhidi ya Afrika Kusini.
Kocha wa DRC, Sebastian Desabre baada ya kupoteza dhidi ya Afrika Kusini. © Pierre René-Worms

Mashindano ya bara kama vile Euro, Kombe la Dhahabu na Kombe la Asia hayachezi mchezo wa mtoano wa nafasi ya tatu. Tangu 2015, waandaaji wa Kombe la Asia walichagua kutoa nafasi ya tatu kwa waliopoteza nusu fainali. Wachezaji wao walifurahia siku moja ya ziada ya mapumziko.

Katika Ligi ya Klabu bingwa barani Ulaya au Afrika, je kuna mchezo wa kuwania nafasi ya tatu?

Wengine wanaweza kubishana kuwa mechi ya mshindi wa tatu inazipa timu nafasi ya mwisho kutafuta ubingwa wa AFCON. Pia, kuna faida ya kifedha kwa mashirikisho kwa sababu ya mchezo wa ziada ambao huzingatiwa wakati wa kuuza haki za upeperushaji kwenye runinga.

Mashabiki wa DR Congo
Mashabiki wa DR Congo © Pierre René-Worms

Lakini pia, mashirikisho yao yangeokoa gharama za usafiri na vifaa pia na kwa mabadiliko ya siku mbili pekee hadi fainali, siku ya ziada ya mapumziko kwa waliofika fainali ingeboresha tukio la onyesho.

Watu wengi na vyombo vya habari pia vinavutiwa na mshindi pekee. Kwa hivyo kusitisha mchujo wa mshindi wa tatu kungeruhusu AFCON kujenga msisimko zaidi kuelekea fainali ya Nigeria dhidi ya Cote d’Ivoire. Timu itakayoshinda inaweza kufurahia umakini wa kipekee wa mashindano wakati wa mizunguko yao ya ushindi na sherehe za medali.

Baada ya yote, ikiwa hakuna mtu anayekumbuka ni nani aliyemaliza wa pili, ni kiasi gani mtu atakumbuka nafasi ya tatu?

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.