Pata taarifa kuu
UN-WAKIMBIZI

Umoja wa Mataifa: Idadi ya wakimbizi duniani yafikia Milioni 80

Idadi ya wakimbizi na watu waliyoyatoroka makaazi yao duniani imezidi kiwango cha watu milioni 80 katikati ya mwaka wa 2020, ikiwa ni rekodi, wakati nchi nyingi zinakabiliwa na janga la COVID-19, Umoja wa Mataifa umesema.

Kambi ya wakimbizi nchini Libya
Kambi ya wakimbizi nchini Libya Picture-alliance/Photoshot
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake, Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi amesema anasikitishwa kwamba ulimwengu umefikia "wakati huu wa giza", na kuonya kuwa hali itakuwa mbaya ikiwa "viongozi wa dunia hawatasitisha vita".

"Jumuiya ya kimataifa inashindwa kulinda amani," amesema, akisisitiza kuwa kuhama kwa lazima kuliongezeka maradufu katika muongo mmoja uliopita.

Mwanzoni mwa mwaka huu, idadi ya watu ambao walikuwa wamelazimika kuyatoroka makaazi yao kwa sababu ya mateso, mizozo na ukiukaji wa haki za binadamu ilifikia Milioni 79.5, na idadi hiyo iliongezeka hadi zaidi ya Milioni 80 kufikia katikati ya mwaka huu wa 2020, kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

Idadi hii ya wakimbizi Milioni 79.5 inajumuisha wakimbizi wa ndani Milioni 45.7, wakimbizi milioni 29.6 na watu wengine waliohamishwa kwa nguvu kutoka nchi zao, na Milioni 4.2 ya watu walitafuta hifadhi katika nchi za kigeni.

"Mizozo iliyopo na mipya pamoja na mlipuko wa Corona vimeathiri sana maisha yao mnamo mwaka 2020," UNHCR imesema katika taarifa.

Licha ya wito wa dharura uliyotolewa mwezi wa Machi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano duniani wakati wa janga hilo, mizozo na mateso vinaendelea, UNHCR imebaini.

Vurugu nchini Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji, Somalia na Yemen vilisababisha watu zaidi kuyatoroka makaazi yao katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka 2020.

Matukio kama hayo pia yameripotiwa katika eneo la katikati mwa Afrika la Sahel, ambapo raia wanakabiliwa na vurugu za kikatili, pamoja na ubakaji na kunyongwa, kulingana na UNHCR.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa kuzuia kuenea kwa COVID-19 zimesababisha ugumu zaidi kwa wakimbizi kupata usalama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.