Pata taarifa kuu

Pakistan: Shule ya pili ya wasichana yalengwa kwa bomu ndani ya wiki moja

Nchini Pakistan, mlipuko uliosababishwa na shambulio kwenye shule ya wasichana ulitokea usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa, Mei 17. Hakuna majeruhi walioripotiwa. Shule iliyolengwa inapatikana kaskazini magharibi mwa Pakistan katika ngome ya zamani ya Taliban ya Pakistani.

Shule ya pili ya wasichana iliyolengwa na bomu ndani ya wiki moja.
Shule ya pili ya wasichana iliyolengwa na bomu ndani ya wiki moja. (Photo : Reuters)
Matangazo ya kibiashara

Hili ni shambulio la pili mwezi huu katika shule ya wasichana katika eneo hili la Pakistan. Kupfikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo. Shule iliyolengwa ilikuwa ikijengwa kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Shambulio hilo lilifanyika katikati ya usiku wakati kulikuwa hakuna mtu hata mmoja katika eneo hilo, anaripoti mwandishi wetu huko Islamabad, Sonia Ghezali.

"Makundi tofauti ya Taliban yanaendesha harakati zao katika eneo hili na wanawatoza fidia wafanyabiashara na wakaazi: wale wanaokataa kulipa wanalengwa, nyumba zao zinaharibiwa au wanauawa," anaelezea afisa mkuu, kwa sharti la kutotajwa jina. Afisa kutoka shirika lisilo la kiserikali la Wana Welfare ambalo husimamia shule iliyolengwa siku ya Alhamisi usiku amebaini kwamba walipokea “barua mwezi mmoja uliopita kutoka kwa kundi lililotuomba sehemu ya pesa zetu. Siku chache baadaye, barua nyingine ilitufikia, ikidai rupia milioni 10," pamoja na "simu za vitisho zilizopigwa kutoka kwa nambari zilizosajiliwa nchini Afghanistan," ameongeza.

Shule nyingine ilishambuliwa mkoani humo

Shambulio hili linakuja siku kadhaa baada ya lingine kama hilo kutokea katika eneo hilo. Shule hizo zinapatikana huko Waziristan, wilaya ya mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, inayopakana na Afghanistan. Miaka michache iliyopita, kundi la Taliban la Pakistani na makundi mengine ya kidini yenye itikadi kali yalikuwa yanaendesha harakati zao katika eneo hili kwa wingi na yalikuwa yamepiga marufuku shule za wasichana.

Elimu ya wasichana imekataliwa kwa muda mrefu na makundi yenye silaha katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP), inayojulikana kwa kumpiga risasi kichwani mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Malala Yousafzai mwaka 2012, miaka miwili baadaye, kwa sababu alitetea wasichana kupata elimu.

Tangu Taliban wachukue mamlaka nchini Afghanistan mnamo mwezi wa Agosti 2021, Taliban wa Pakistani, ingawa ni kundi tofauti, wana itikadi sawa. Pakistan tangu wakati huo imekabiliwa na kuzorota kwa usalama, haswa katika mikoa ya mpakani.

Mashambulizi haya yanakumbusha miaka mibaya zaidi ya ugaidi

Kundi la Taliban wamepata ushawishi tena kaskazini-magharibi mwa Pakistan na wanaongeza mashambulizi, haswa dhidi ya vikosi vya usalama na wawakilishi wa serikali. Mashambulizi mengi hufanywa na TTP, kundi tofauti na Taliban ya Afghanistan lakini inayoendeshwa na itikadi sawa. Taliban hawa pia ni wa kwanza kushukiwa kuwa nyuma ya mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya shule za wasichana.

Matukio haya yanakumbusha miaka mibaya zaidi ya ugaidi nchini Pakistani, hasa kufungwa kwa shule za wasichana kulikoamriwa mwaka 2009 na Mullah Fazlulah. Kiongozi huyu wa Taliban alikuwa amechukua udhibiti wa bonde la Swat katika eneo hilo na kutawala ugaidi na wapiganaji wake wenye silaha ambao walikuwa wameweka toleo kali la sheria ya Kiislamu, Sharia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.