Pata taarifa kuu
USALAMA-UCHUMI

Masisi: Waasi wa M23 wanadhibiti mji wa Rubaya

Waasi wa M23, wakiungwa mkono na jeshi la Rwanda kulingana na vyanzo mbalimbali vikinukuliwa na Radio OKAPI, wamedhibiti mji wa madini wa Rubaya, eneo la Masisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini, tangu Jumanne Aprili 30.

Raia wa DRC wanatoroka eneo la Masisi, kwenye barabara karibu na Saké, Februari 7, 2024.
Raia wa DRC wanatoroka eneo la Masisi, kwenye barabara karibu na Saké, Februari 7, 2024. AFP - AUBIN MUKONI
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa idara ya madini katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Yvette Mwanza, anathibitisha kuwa kutokana na uvamizi wa mgodi huu, mapato makubwa hayataingia katika hazina ya serikali.

Kulingana afisa huyo, mgodi wa Rubaya ndio kitovu cha uchumi wa sekta ya madini huko Kivu Kaskazini katika suala la mapato ya mkoa:

"Uzalishaji wa Coltan katika Rubaya pekee unawakilisha 50% ya uzalishaji wa kitaifa."

Watu mbalimbali nchini DRC wanajaribu kupaza sauti kulaani uporaji, unyonyaji na uuzaji haramu wa madini kutoka eneo hili la uchimbaji madini.

Baadhi ya waangalizi hata wanabaini kwamba kukaliwa kwa mji wa madini wa Rubaya na M23 kunafungua njia ya uchimbaji haramu wa madini.

Eneo la Rubaya lina madini kadhaa ikiwa ni pamoja na coltan, manganese, cassiterite na tourmaline.

Kulingana na wataalamu katika sekta ya madini, madini yanayozalishwa Rubaya huwa hayanufaishi taifa la Kongo kwa sababu yanachimbwa na kusafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria na baadhi ya wanamgambo ambao hupanga usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani, ambayo ni upungufu kwa hazina ya umaa.

Pia wanabaini kwamba kwa muda mgodi wa Rubaya pia umekuwa ukitamaniwa na makampuni ya kigeni yanayojaribu kukwepa kodi.

Katika barua yake ya Aprili 26, Waziri wa Madini, Antoinette N'Samba aliidhinisha shirika la wachimbaji madini wa Kongo (CDM) kuanzisha harakati ya kusimamia uchimbaji madini kwa sababu wamepata kibali cha kufanya kazi, kwa nia ya kuwaleta pamoja wachimbaji wadogo na kuwaunganisha wote kwa uzalishaji wao.

Wasiwasi wa wakazi wa eneo la Rubaya

Baada ya kumiliki Rubaya, waasi hawa walichukua udhibiti wa maeneo ya Kibabi na Kitanda, huko Masisi.

Hali hii inatia wasiwasi mashirika ya kiraia. Ripota wake, Télesphore Mitondeke anaonyesha kuwa washambuliaji hawa wanasonga mbele kuelekea eneo la Katale, Ngungu na Kinigi, kwa mwelekeo wa maeneo ya Ufamando ya kwanza na Katoyi.

"Hali inasalia kuwa ya wasiwasi kwa sababu adui anaendelea kukaribia mji mkuu wa eneo la Masisi. Hatua za kiusalama itabidi zichukuliwe ili kukabiliana na mzozo huu,” amesema kulingana na Radio OKAPI.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.