DR Congo yasonga mbele michuano ya AFCON, Tanzania yafungishwa virago
Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imefuzu katika hatua ya 16 bora, kuwania kombe la mataifa ya Afrika, baada ya kutofungana na Tanzania kwenye mechi ya mwisho ya hatua makundi, Jumatano usiku.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Cheza - 01:39
Matokeo hayo, yameiondoa Tanzania kwenye michuano hiyo baada ya kumaliza kundi la F kwa alama 2. Taifa Stars ilianza vibaya baada ya kufungwa na Morocco mabao 3-0 na ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia.
Mara tatu ambayo imecheza michuano hii mikubwa barani Afrika 1980, 2019 na 2023 haijawahi kushinda mechi yoyote.
Ushindi wa Morocco wa bao 1-0 dhidi ya Zambia, iliisaidia wenyeji Cote Dvoire kusonga mbele kama mojawapo ya timu iliyomaliza katika nafasi ya tatu bora katika kundi la A.
Katika hatua nyingine, kocha wa Tunisia Jalel Kadri, ametangaza kujiuzulu baada ya timu yake kuondolewa kwenye michuano hiyo.
“Naondoka kwa sababu mkataba wangu ulinitaka nifike kwenye hatua ya nusu fainali, kwa sababu hatujafikia hapo, mkataba wangu umekwisha,” amesema.
Tunisia imeondoka kwenye michuano hiyo, bila ya kushinda hata mechi moja katika kundi E.
Ameugana na makocha wa wenyeji Cote Dvoire, Ghana na Algeria ambao wameachishwa kazi wiki hii kwa sababu ya matokeo mabaya.
Ratiba ya hatua ya 16 bora
Jumamosi 27/01/2024
- Angola vs Namibia
- Nigeria vs Cameroon
Jumapili 28/01/2024
- Equatorial Guinea vs Guinea
- Misri vs Congo DR
Jumatatu 29/01/2024
- Cabo Verde vs Mauritania
- Senegal vs Côte d'Ivoire
Jumanne 30/01/2024
- Mali vs Burkina Faso
- Morocco vs Afrika Kusini