Pata taarifa kuu
FAINALI ZA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA

Michezo 13 ya kusaka kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika yachezwa

Michezo 13 ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za Mwaka 2013 ambazo zitafanyika nchini Afrika Kusini imepigwa kwenye viwanja mbalimbali jana kabla ya marudiano kufanyika mwezi wa sita mwaka huu.

Uwanja wa Taifa wa Tanzania uliochezwa mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Msumbiji
Uwanja wa Taifa wa Tanzania uliochezwa mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Msumbiji
Matangazo ya kibiashara

Tanzania inayotambulika kama Taifa Stars ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa ikaambulia sare ya goli 1-1 mbele ya Msumbiji inayojulikana kwa jina la Utani kama The Mambas.

Msumbiji ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli kabla ya Taifa Stars hawajaja juu na kufanikiwa kusawazisha goli hilo katika kipindi cha kwanza matokeo ambayo yalisalia hadi mwisho wa mchezo huo.

Kenya wanaofahamika kama Harambee Stars wakiwa nyumbani wakafanikiwa kuibuka washindi mbele ya Togo kwa kuwafunga kwa magoli 2-1 na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuweza kusonga mbele kwenye hatua nyingine.

Uganda maarufu kama The Cranes wao wakakutana na balaa baada ya kujikuta wakipoteza mchezo wake dhidi ya Congo Brazaville kwa kuchabangwa magoli 3-1 kwa hiyo kuwa na kibarua kizito katika mchezo wa marudiano.

Leopards ambayo ni Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC yenyewe imejiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kushinda mchezo wake wa ugenini dhidi ya Ushelisheli kwa magoli 4-0.

Burundi maarufu Inamba Murugamba wakafanikiwa kuchomoza na ushindi kwenye mchezo wao mbele ya Zimbabwe kwa magoli 2-1 lakini wamepatwa na pigo baada ya kocha wake Adel Amrouch kutangaza kujiuzulu.

Cameroon maarufu kama Simba Wasiofugika wakapata ushindi wa dakika za lala salama wa goli 1-0 dhidi ya Guinea-Bissau huku Madagascar wakikumbana na kichapo kizito cha magoli 4-0 mbele ya Cape Verde.

Matokeo megine yanaonesha Ethiopia ilikwenda sare ya bila kufungana na Benin wakati Rwanda wakiwabana mbavu Nigeria na kumaliza dakika tisini bila kufungana nao huku Chad wakiwafunga Malawi kwa magoli 3-2.

Liberia wao wakapata ushindi wa goli 1-0 mbele ya Namibia huku Algeria wakiwafunga Gambia kwa magoli 2-1.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.