Pata taarifa kuu

Kenya yawekwa katika tahadhari kabla ya kuwasili kwa kimbunga cha kwanza katika historia yake

Rais wa Kenya William Ruto siku ya Ijumaa aliiweka nchi yake iliyokumbwa na mafuriko katika hali ya tahadhari na kuahirisha kufunguliwa kwa shule kwa muda usiojulikana, huku raia wakijiandaa kuwasili kwa kimbunga cha kwanza kabisa nchini katika historia yake.

Idadi ya vifo tangu mwezi Machi nchini Kenya imezidi 200, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imetangaza siku ya Ijumaa. Zaidi ya watu 165,000 wameyakimbia makazi yao na karibu watu 100 hawajulikani walipo nchini humo.
Idadi ya vifo tangu mwezi Machi nchini Kenya imezidi 200, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imetangaza siku ya Ijumaa. Zaidi ya watu 165,000 wameyakimbia makazi yao na karibu watu 100 hawajulikani walipo nchini humo. AP - Patrick Ngugi
Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya watu 350 wamekufa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Afrika Mashariki tangu mwezi Machi na eneo hilo sasa linatishiwa na kimbunga kinachotarajiwa kupiga mwishoni mwa juma hili katika ufuo wa Bahari ya Hindi.

"Kimbunga hiki, kwa jina Hidaya, ambacho kinaweza kupiga wakati wowote sasa, kinatarajiwa kuleta mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi yenye nguvu na hatari," Rais Ruto amesema katika mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi.

"Nchi yetu lazima ichukue hatua haraka na kwa uthabiti kupunguza athari mbaya za mzozo wa sasa na kulinda maishaya watu na mali," ameongeza.

Ufunguzi wa shule, uliopangwa siku ya Jumatatu, uliahirishwa na mawaziri wote wakaagizwa kuratibu uhamishaji na upangaji wa makazi ya Wakenya walioathiriwa. Kimbunga Hidaya kitafikia kilele kwa kasi ya kilomita 165 kwa saa kitakapotua katika nchi jirani ya Tanzania siku ya Jumamosi, kulingana na kituo cha hali ya hewa ICPAC.

Msimu wa vimbunga kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa kawaida huanza mwezi Novemba hadi mwezi Aprili na hushuhudia karibu dhoruba kumi na mbili kila mwaka. Siku ya Ijumaa mamlaka ya Tanzania imeonya kwamba mfumo wa hali ya hewa uitwayo Hidaya "umeimarika kufikia hadhi ya kimbunga kikubwa" saa 3 asubuhi kwa saa za ndani kilipokuwa kilomita 400 kusini mashariki mwa mji wa Mtwara. "Kimbunga Hidaya kiliendelea kuimarika, huku upepo ukifika kilomita 130 kwa saa," walisema katika taarifa ya utabiri wa hali ya hewa.

Mvua katika eneo hilo imeongezwa na El Niño, mfumo wa hali ya asili ya hewa inayohusishwa kwa ujumla na ongezeko la joto duniani, ambalo husababisha ukame katika baadhi ya maeneo ya dunia na mvua kubwa mahali pengine.

Mvua zinazoendelea kunyesha zilikumba nchi nyingi za Afrika Mashariki, na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo yaliharibu mazao, kusomba nyumba na kusababisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Idadi ya vifo tangu mwezi Machi nchini Kenya imezidi 200, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imetangaza siku ya Ijumaa. Zaidi ya watu 165,000 wameyakimbia makazi yao na karibu watu 100 hawajulikani walipo nchini humo.

"Hakuna sehemu yoyote ya nchi yetu ambayo imeepushwa na uharibifu huu," Rais Ruto amesema. "Kwa bahati mbaya, hatujaona mwisho wa kipindi hiki hatari," ameonya. Takriban watu 155 wamefariki katika mafuriko sawa na hayo katika nchi jirani ya Tanzania.

Katika mvua iliyonyesha, waokoaji walikimbia dhidi ya wakati kusaidia watu waliokwama na mafuriko nchini Kenya. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilimuokoa mwanamume aliyesema kuwa alikuwa amezingirwa na mafuriko na kulazimika kujihifadhi juu ya mti kwa siku tano huko Garissa, mashariki mwa nchi, kulingana na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatano.

Jeshi pia lilijiunga na shughuli za kutoa misaada ya kuwaondoa watu wote wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

Siku ya Alhamisi Serikali pia iliamuru mtu yeyote anayeishi karibu na mito mikubwa au karibu na "mabwawa au hifadhi 178 zilizojaa au karibu kujazwa maji" kuhama eneo hilo ndani ya saa 24.

Nchini Burundi, takriban watu 29 wamefariki na 175 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa msimu wa mvua mwezi Septemba, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema "ana wasiwasi hasa" kuhusu hatima ya maelfu ya wakimbizi waliokimbia makazi yao nchini Burundi, Kenya, Somalia na Tanzania. "Wanalazimika kukimbia kwa mara nyingine kuokoa maisha yao baada ya nyumba zao kusombwa na maji," msemaji wa UNHCR Olga Sarrado Mur amesema siku ya Ijumaa.

Mwishoni mwa mwaka 2023, mvua kubwa iliyonyesha nchini Kenya, Somalia na Ethiopia ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 300, katika eneo ambalo lilikuwa likijitahidi kujikwamua kutokana na ukame mbaya zaidi kuwahi kuripotiwa katika kipindi cha miaka 40.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.