Pata taarifa kuu
CHINA-UINGEREZA-HONG KONG-USALAMA-USHIRIKIANO

Hong Kong: Beijing yaitishia Uingereza kukabiliwa na hatua kali

China imeonya juu ya "athari" ya uamuzi wa Uingereza kusitisha mkataba wake wa kubadilishana watuhumiwa na Hong Kong, katika kupinga sheria tata ya usalama wa kitaifa katika koloni la zamani la Uingereza, la Hong Kong.

Bendera ya China kwenye makao makuu ya Usalama wa Taifa huko Hong Kong, Julai 8, 2020.
Bendera ya China kwenye makao makuu ya Usalama wa Taifa huko Hong Kong, Julai 8, 2020. AFP
Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo, iliyochukuliwa Jumatatu wiki hii, inatishia kuvunja uhusiano kati ya China na Uingereza ambao tayari umedorora, wakati Uingereza imeamua kupiga marufuku vifaa vyote vya kampuni ya simu kutoka China ya Huawei 5G kwa mitandao yake na wanasiasa waliikosoa China kwa kukandamiza jamii za watu wachache katika Jimbo la Xinjiang.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Ubalozi wa China nchini Uingereza imekosoa uamuzi wa Uingereza kusitisha mkataba huo na kubaini kwamba "upande wa Uingereza unakwenda mbali zaidi katika mwelekeo mbaya".

"China inautaka upande wa Uingereza kuacha mara moja kuingilia maswala ya Hong Kong ambayo ni maswala ya ndani ya China," imesema taarifa hiyo ya msemaji wa ubalozi wa China.

"Uingereza itakabiliwa na athari ikiwa itasisitiza kwenda kwenye njia mbaya," taarifa hiyo imeongeza.

Hatua hii ya Uingereza kusitisha mkataba wa kubadilishana watuhumiwa inakuja baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Marekani, Canada na Australia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Dominic Raab amethibitisha uamuzi huo bungeni jana Jumatatu licha ya Beijing kujibu kuwa hatua hiyo ni kosa kubwa la sera za kigeni na hatari ya kulipiza kisasi.

"Serikali imeamua kusitisha mkataba wa kubadilishana watuhumiwa mara moja na kwa muda usiojulikana," Raab amesema.

Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kuongezeka kati ya Uingereza na Beijing, waziri mkuu Boris Johnson amesema ana hofu kuhusu sheria mpya na madai ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini China na hususan namna inavyoichukulia jamii ya Waislamu walio wachache wa Uighur. Johnson aliahidi kuchukua hatua kali, lakini akisema haitamaanisha kuachana kabisa na sera ya

kimahusiano na China.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.