Uingereza imesema idadi ya waomba hifadhi watakaotumwa Rwanda ni ndogo
Nairobi – Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereaza, juma hili amesema kuwa huenda idadi ya wahamiaji watakaofukuzwa nchini humo chini ya makubaliano na nchi ya Rwanda, ikawa ndogo lakini itategemea na mambo mengine yatakayojitokeza.
Imechapishwa:
Cheza - 00:48
Waziri, James Cleverly, amewaambia wabunge kuwa makubaliano na taifa hilo la Afrika mashariki ni "sehemu moja tu" ya majibu ya serikali katika kukabiliana na uhamiaji haramu, akidai pia mikataba na nchi nyingine inaweza kuwa na "athari" kwa idadi itakayotumwa.
Hata hivyo, licha ya shinikizo kutoka kwa wabunge waliotaka kufahamu ni wahamiaji wangapi watapelekwa nchini Rwanda, waziri Cleverly, alikataa kutabiri ni watu wangapi wangefukuzwa na kwamba bado hawajukubaliana na Kigali kuhusu idadi yao.
Kauli yake anaitoa wakati huu maswali kuhusu gharama ya mpango huo yakiongezeka baada ya kuibuka mwezi uliopita kuwa Uingereza imelipa pauni milioni 240 kwa Rwanda, licha ya mizozo ya kisheria, ikimaanisha kuwa bado hakuna mtu aliyepelekwa Rwanda.
Sheria ya kufufua mpango huo baada ya kuamuliwa kuwa ni kinyume cha sheria na mahakama ya juu ilipitishwa na wabunge mapema mwezi huu, lakini inatarajiwa kupata upinzani mkubwa katika bunge la wananchi.
Chini ya mpango huo wa miaka mitano, Uingereza itatuma idadi ambayo haijabainishwa ya wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda - ambapo wanaweza kutuma maombi ya kuwa mkimbizi wakiwa huko au kutafuta hifadhi katika "nchi nyingine ya tatu ambayo ni salama".