Pata taarifa kuu
HAKI-SHERIA

Somalia: Mwandishi wa habari, aliyeachiliwa hivi majuzi, afungwa tena

Mwandishi wa habari wa kujitegemea nchini Somalia, aliyeachiliwa mwezi Februari baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi miwili jela kwa kutishia usalama wa taifa, amefungwa tena, chama cha waandishi wa habari kimeliambia shirik la habari la AFP siku ya Jumatano.

Ikulu ya rais mjini Mogadishu, Somalia, tarehe 28 Desemba 2021.
Ikulu ya rais mjini Mogadishu, Somalia, tarehe 28 Desemba 2021. © FEISAL OMAR / REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Abdalle Ahmed Mumin, pia katibu mkuu wa chama cha Waandishi wa Habari wa Somalia (SJS), alikamatwa mwezi Oktoba, muda mfupi baada ya uamuzi wa serikali wa kuimarisha ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari, akishutumiwa kushiriki katika propaganda za Waislam wenye itikadi kali Al Shabab. Mnamo mwezi Februari, mahakama ilimhukumu Abdalle Ahmed Mumin kifungo cha miezi miwili jela lakini aliachiliwa mara baada ya hapo, uamuzi ambao uliwashangaza wengi.

Ofisi ya mwanasheria mkuu ilisema Jumanne kwamba kuachiliwa huko hakukuwa na msingi wa kisheria na ilisema katika taarifa kwamba "vikosi vya polisi vya Somalia, kufuatia amri ya mahakama vilimrudisha (Abdalle Ahmed Mumin) gerezani mnamo Februari 23". Mohamed Ibrahim, rais wa SJS, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "kukamatwa tena kwa Abdalle Ahmed Mumin, katibu mkuu wa SJS, ni kinyume cha sheria".

“Tunalaani uamuzi huo na tunaomba aachiliwe huru,” amesema. Mwishoni mwa mwaka 2022,chama cha Waandishi wa habari cha SJS na makundi mengine manne ya utetezi wa vyombo vya habari vilipinga uamuzi wa serikali kukandamiza zaidi vyombo vya habari, vikisema kuwa utaminya uhuru wa kujieleza.

Shirika lisilo la kiserikali la Waandishi wasio na mipaka (RSF) linaiweka Somalia katika nafasi ya 140 (kati ya nchi 180) katika orodha yake ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huku zaidi ya waandishi 50 wakiuawa nchini humo tangu mwaka 2010.

Kulingana na RSF, Somalia (wakazi milioni 17) ni nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari barani Afrika. Kimsingi wanatishiwa na Al Shabab kundi lenye uhusiano na Al-Qaeda ambalo linajaribu kupindua serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, lakini mamlaka pia inashutumiwa kwa kukiuka haki zao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.