Pata taarifa kuu

DRC: Wafungwa 66 wafariki katika kipindi cha miezi miwili katika gereza la Makala mjini Kinshasa

Wafungwa 66 wamefariki tangu Januari 1 huko Makala, gereza kuu katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, kwa sababu ya mazingira ambamo wanazuiliwa, kulingana na kiongozi wa shirika moja la haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gereza la kiraia la Makala mjini Kinshasa, DRC, ambapo wafungwa 66 wamefariki tangu Januari 1, 2023.
Gereza la kiraia la Makala mjini Kinshasa, DRC, ambapo wafungwa 66 wamefariki tangu Januari 1, 2023. AFP PHOTO / JUNIOR D. KANNAH
Matangazo ya kibiashara

Wafungwa hao walifariki kwa utapiamlo, kukosa hewa, au kukosa huduma, mwanaharakati Emmanuel Cole, mtetezi wa haki za wafungwa ambaye hutembelea magereza mara kwa mara, ameliambia shirika la habari la AFP.

Siku ya Jumapili, "wafungwa wawili walifariki katika gereza la Makala, mimi mwenyewe niliona miili yao", ameongeza. Wafungwa hawa wawili wapya ambao walifariki kutokana na mazingira ambamo walikuwa wanazuiliwa, wanafikisha idadi ya vifo kufikia 35 kwa mwezi wa Februari pekee, kulingana na Bw. Cole.

Mnamo mwezi Januari, shirika lake liliweza kuorodhesha "watu 31 waliofariki ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja", katika jela la Makala. Jela hili ambalo lilijengwa wakati wa enzi za ukoloni kwa uwezo wa kupokea watu 1,500, kwa sasa lina wafungwa 10,790, wakiwemo 7,780 walio katika kizuizi cha muda, amesema Bw. Cole, ambaye hufuatilia hali ya wafungwa kila siku.

Tangu mwanzoni mwa mwaka, mamlaka ya mahakama imeruhusu kuachiliwa kwa masharti kwa wafungwa 635 ili kupunguza idadi ya wafungwa katika jela, amesema Bw. Cole, akithibitisha habari kutoka kwa vyombo vya habari vya DRC.

Chakula kinachotolewa kwa wafungwa siyo tu "hakitoshi" bali pia kina "ubora duni", wakati "kula kunapaswa kuwa haki kwa kila mfungwa", amebaini. Akiwa madarakani tangu Januari 2019, Rais wa DRC Felix Tshisekedi alisifu rekodi yake ya haki za binadamu Jumatatu wakati wa hotuba katika Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva, Uswisi.

Bw. Tshisekedi anasema "ameweka ulinzi na uendelezaji wa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi miongoni mwa vipaumbele vya mamlaka (yake) na serikali ya Jamhuri".

“Tunaziomba mamlaka kuharakisha taratibu ili kutoweka mahabusu mamia na hata maelfu ya watu kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani wala kuhukumiwa,” amesema Emmanuel Cole.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.