Pata taarifa kuu

DRC: Mapigano mapya yazuka karibu na Ntamugenga kati ya FARDC na M23

Mapigano yaliendelea Jumapili katika eneo la Rutshuru, Kivu Kaskazini, kati ya wapiganaji wa FARDC na M23. Mapigano haya mapya yaliyoanza tangu Alhamisi, Oktoba 20 yamesababisha watu wengine kuhama makazi yao, hasa katika eneo la Ntamugenga linalozozaniwa na pande hizi mbili.

Wanajeshi wa jeshi la Kongo wakishika doria karibu na Kiwanja mnamo Aprili 3, 2022 siku chache baada ya mapigano na waasi wa M23 huko Rutshuru.
Wanajeshi wa jeshi la Kongo wakishika doria karibu na Kiwanja mnamo Aprili 3, 2022 siku chache baada ya mapigano na waasi wa M23 huko Rutshuru. AFP - GUERCHOM NDEBO
Matangazo ya kibiashara

Mapigano mapya yalizuka katika vijiji viwili katika eneo la Rutshuru. Mapigano yaliripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye barabara ya Rangira-Rwanguba-Tchengerero. Lengo la M23, linasema jeshi, lilikuwa kuzuia barabara zinazotumiwa na vikosi vya FARDC. Baada ya makabiliano makali, jeshi linasema liliwarudisha nyuma waasi na kuwakamata baadhi yao.

Mpigano mengine yaliripotiwa katika eneo la Ntamugenga. Makombora yalianguka katika maeneo yanayokaliwa na watu, ikiwa ni pamoja na eneo la makasisi, na kusababisha vifo vya watu kadhaa na majeruhi wengi, kulingana na vyanzo vya ndani. Duru za kijeshi ambazo hazikutaka kutajwa jina zinasema kuwa jeshi lilikataa kupigana katikati ya eneo lenye watu wengi ili kuepusha uharibifu mkubwa. Jumatatu asubuhi, utulivu ulirejea katika eneo linalokaliwa na waasi wa M23.

Wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu

Shirika la kimataifa la matibabu na kibinadamu la Médecins sans frontières (MSF) limetoa wito wa kufunguliwa kwa eneo la usalama la kibinadamu ili kuwaondoa raia na waliojeruhiwa. "Tuna wasiwasi sana kuhusu hali ya kibinadamu huko Ntamugenga," amesema Bénédicte Lecoq, msimamizi wa dharura wa MSF katika eneo la Rutshuru.

Inatarajiwa kwamba eneo hilila usalama la kibinadamu itaweza kufunguliwa ili kuweza kuwaondoa majeruhi hawa kwa haraka sana na pia raia ambao wamekwama katika kijiji hiki.

Takriban watu 23,000 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizi za silaha tangu Oktoba 20, inaripoti kwa upande wake Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA). Kulingana na chanzo hicho, takwimu hizi zinajumuisha takriban watu 2,500 waliovuka mpaka na kuingia Uganda. Na kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano haya yanafanya jumla ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo la Rutshuru kufikia zaidi ya 396,000.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.