Pata taarifa kuu
DRC-USALAMA

Mashirika ya kiraia Uvira yalaani uvamizi wa wanajeshi wa Burundi DRC

Mashariki mwa DRC, katika mkoa wa Kivu Kusini, mashirika ya kiraia katika mji na eneo la Uvira yanalaani ukiukaji mwingine wa mpaka wa DRC unaofanywa na askari wa jeshi la Burundi kwa zaidi ya wiki moja, katika kuwasaka waasi wa Burundi wa RED-Tabara, wanaopiga kambia katikati na nyanda za juu huko Uvira, karibu na mpaka wa Burundi.

Mji wa Uvira nchini DRC.
Mji wa Uvira nchini DRC. Photo MONUSCO/Abel Kavanagh
Matangazo ya kibiashara

Wakati huu, takriban wanajeshi 400 wa jeshi la Burundi wanasemekana kuingia nchini DRC kuanzia Desemba 23, kupitia Mto Ruzizi kaskazini mwa Uvira. Kwa mujibu wa afisa mkuu wa Burundi, baadhi ya askari hao ni kutoka kikosi cha 212 cha makomandoo kilichopo kwenye msitu wa Rukoko karibu na mpaka wa DRC, wengine wanatoka vitengo viwili vya kiso maalum, BSPI, aina ya kikoi cha walinzi wa rais, na polisi wa jeshi la Burundi.

Wanamgambo kutoka chama tawala nchini Burundi pia wanaripotiwa kuingia nchini DRC, kama kawaida katika operesheni kama hizo.

Waliendelea kwa wiki moja katikati na nyanda za juu zinazotazamana na Uvira, kabla ya kuanza mashambulizi yao dhidi ya ngome za waasi wa Burundi wa RED-Tabara katika eneo la Bijombo, siku tatu zilizopita, kulingana na mashirika ya kiraia huko Uvira. Makundi haya ya waasi yamekuwepo katika eneo hilo kwa miaka kumi na mara kwa mara yanadai mashambulizi nchini Burundi. Mashambulizi ya hivi karibuni yalifanyika siku mbili kabla ya uvamizi huu, uvamizi uliothibitishwa na RFI na chanzo cha usalama cha Burundi.

Baadhi ya wajumbe wa mashirika hayo wanadai kulitahadharisha jeshi la DRC mara tu wanajeshi walipoingia nchini, lakini zaidi ya wiki moja baadaye, msemaji wa FARDC katika eneo hilo alihakikisha kwamba uchunguzi bado unaendelea. "Kuna makundi yenye silaha yanayotoka mataifa ya kigeni ambayo yanajipenyeza katika ardhi ya DRC. Lakini kusema kwamba ni jeshi la Burundi, siwezi kuthibitisha au kukanusha. Kuna mapigano kati ya makundi haya yenye silaha ”, amesema Meja Dieudonné Kasereka.

Baada ya takriban siku tatu za mapigano, waasi wa Burundi wa RED-Tabara walitangaza kuwa wamewaua takriban wanajeshi kumi wa Burundi. Kwa upande wake, jeshi la Burundi halijazungumza kuhusiana na madai hayo.

Mashirika ya kiraia huko Uvira yanalaani mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi kuingizwa katika ardhi ya DRC, pia yanashutumu jeshi la DRC, FARDC, kwa kufumbia macho jambo hilo kwa sababu, bila shaka, kwa makubaliano ya siri kati ya Gitega na Kinshasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.