Pata taarifa kuu
BURUNDI-RPA-SIASA-SHERIA

Mkurugenzi wa redio RPA, aombwa dhamana

Afisa wa Mashitaka katika Mahakama ya rufaa mjini Bujumbura, nchini Burundi ameomba dhamana ya kuachiliwa kwa muda mkurugenzi wa redio RPA, Bob Rugurika, ambaye anazuiliwa katika jela kuu la mkoa wa Muramvya.

Jengo la redio RPA mjini Bujumbura.
Jengo la redio RPA mjini Bujumbura. http: //www.rpa-burundi.org/
Matangazo ya kibiashara

Afisa huyo wa Mashitaka ameomba majaji kumuachilia huru mkurugenzi wa RPA iwapo atakubali kutoa dhamana ya milioni 20 franka za Burundi sawa  na zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 7, au kumfikisha mikononi mwa vyombo vya sheria mtu aliyekubali mwenyewe kupitia redio RPA, kwamba alitumiwa na baadhi ya vigogo katika polisi na Idara ya ujasi kwa ushirikiano na wenzake, kuwamalizia maisha watawa watatu kutoka Italia, mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka 2014 wilayani Kamenge, kaskazini mashariki mwa mji wa Bujumbura.

Mkurugenzi wa redio RPA, Bob Rugurika alifikishwa mbele ya majaji kwa mara ya pili Jumatatu Februari 16, katika jela kuu la mkoa wa Muramvya, nchini Burundi, ili kujua iwapo atendelea kusikilizwa akiwa huru au atasalia jela.

Uamzi wa majaji utatolewa ndani ya masaa 48 kuanzia Jumatatu wiki hii, baada ya majaji kumsikiliza.

Mmoja kati ya wanasheria wa mkurugenzi huyo wa redio RPA, Fabien Segatwa amesema ana imani kuwa mteja wao ataachiliwa huru, ili aendelee kusikilizwa akiwa huru.

Hivi karibuni Umoja wa Ulaya na Marekani viliitolea wito serikali ya Burundi kumuachilia huru haraka iwezekanavyo mwanahabari huyo.

Wabunge wa Umoja wa Ulaya wametishia kuichukulia Burundi vikwazo iwapo haitomuachilia huru mwanahabari huyo. Wabunge hao walipitisha hivi karibuni azimio la kusimamisha msaada wa Yuro milioni 450 ambao wangeliitolea Burundi.

Jumatano februari 4 mwaka 2015, majaji wa mahakama ya jiji la Bujumbura katika hatua ya kwanza walichukua uamzi wa kumbakiza jela mwanahabari Bob Rugurika, akiwa pia mkurugenzi wa redio RPA, inayosikilizwa na watu wengi nchini Burundi na baadhi ya maeneo ya nchi jirani.

Hata hivyo Umoja wa Ulaya, Marekani na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu wameitaka serikali kumuachilia huru mwanahabari huyo, kwani hana hatia, huku wakiomba uchunguzi uanzishwe kuhusu watawa 3 kutoka Italia waliouawa mwanzoni mwa mwezi Septemba.

Bob Rugurika alikamatwa na kupelekwa katika jela kuu la Mpimba mjini Bujumbura, Jumanne Januari 20 jioni, baada ya kuitika hati iliyotolewa na afisa katika Ofisi ya mwendesha mashitaka katika manispaa ya jiji la Bujumbura, Emmanuel Nkurikiye, ambaye alimtaka amfikishe mikononi mwa vyombo vya sheria, mtu aliyekiri kuhusika na mauaji ya watawa watatu kutoka Italia waliouwawa tarehe 7 na 8 Septemba mwaka 2014, katika wilaya ya Kamenge, kaskazini mashariki mwa mji wa Bujumbura.

Redio RPA iliendesha uchunguzi kuhusu mauaji hayo, na kwa muda wawiki kadhaa redio hio ilikua ikiweka wazi matokeo ya uchunguzi wake, ambapo mtu huyo aliyekiri kuhusika katika mauaji hayo, aliwanyooshea kidole baadhi ya maafisa wakuu katika Idara ya Ujasusi ya Burundi pamoja na polisi, akibaini kwamba wao ndio waliomuagiza akishirikiana na watu wengine (ambao aliwataja majina) kutekeleza mauaji ya watawa hao.

Mtu huyo aliyehojiwa na redio RPA, alimtaja mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Burundi, jenerali Adolphe Nshimirimana, akibaini kwamba ni mmoja kati ya maafisa wa Idara ya Ujasusi na polisi walioandaa mpango huo wa kuwamalizia maisha watawa hao kutoka Italia.

Hata hivyo katika uchunguzi wake, RPA ilibaini kwamba ilijaribu kuwatafuta watu wote waliotajwa katika kesi hiyo, baadhi walikanausha tuhuma dhidi yao, na wengine walisema kwamba wanasubiri uchunguzi wa vyombo vya sheria vya Burundi.

Afisa wa Ofisi ya mashitaka anamtuhumu Bob Rugurika kwamba hakutoa ushiriki wake kwa vyombo vya sheria, kuingilia kazi za vyombo vya sheria wakati kesi ikiwa katika hatua ya uchunguzi, na kushiriki katika mauaji ya watawa hao watatu kutoka Italia.
Mkurugenzi wa redio RPA anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela, iwapo atapatikana na hatia.

Baada ya mauaji ya watawa hao, polisi ya Burundi ilimkamata mtu anayedaiwa kuwa mgonjwa wa akili, ikimtuhumu kuhusika katika mauaji ya watawa watatu waliouawa tarehe 7 na 8 septemba mwaka 2014 wilayani Kamenge mjini Bujumbura.

Picha ya Christian Butoyi, mwenye umri wa mika 33, anaedaiwa kuwaua watawa watatu kutoka Italia, wakati akionyeshwa na polisi mbele ya vyombo vya habari mjiniBujumbura, Septemba 9 mwaka 2014.
Picha ya Christian Butoyi, mwenye umri wa mika 33, anaedaiwa kuwaua watawa watatu kutoka Italia, wakati akionyeshwa na polisi mbele ya vyombo vya habari mjiniBujumbura, Septemba 9 mwaka 2014. RFI/Esdras Ndikumana

Redio RPA imekua ikiendelea kurusha matokeo ya uchunguzi wake, licha ya kuwa mkurugenzi wake anazuiliwa jela.

Kanisa Katoliki nchini Burundi iliomba hivi karibuni mkurugenzi huyo wa redio RPA aachiliwe huru, huku ikiomba vyombo vya sheria vya Burundi kuanzisha uchunguzi wa kina ili waliohusika katika mauaji ya watawa watatu kutoka Italia wajulikane, na waadhibiwe kwa mujinu wa sheria.

Hivi karibuni mwakilishi wa Papa Francis nchini Burundi, mabalozi wa Ulaya na marekani walimtembelea mkurugenzi huyo wa redio RPA, katika jela anakozuiliwa, mkoani Muramvya, katikati mwa Burundi, na kuomba aachiliwe huru.

Baraza la Maaskofu wa Kanisa katoliki nchini Burundi.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa katoliki nchini Burundi. Esdras Ndikumana / RFI

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.