Pata taarifa kuu

Uingereza: Rishi Sunak anakuwa Waziri Mkuu rasmi

Rishi Sunak ambaye amepewa majukumu  na Mfalme Charles III ya kuunda serikali, aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Jumanne, ikiwa ni kiongozi wa tatu wa serikali katika kipindi cha miezi miwili, katika nchi iliyotumbukia katika mzozo mkubwa wa kiuchumi na kijamii.

Rishi Sunak amepokelewa na Mfalme Charles III na akawa Waziri Mkuu wa Uingereza rasmi tarehe 25 Oktoba 2022.
Rishi Sunak amepokelewa na Mfalme Charles III na akawa Waziri Mkuu wa Uingereza rasmi tarehe 25 Oktoba 2022. © Aaron Chown/Pool via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Mfalme Charles III alimwagiza Rishi Sunak kuunda serikali mnamo Jumanne, Oktoba 25. Mfanyabiashara huyo wa zamani wa benki na Waziri wa Fedha hivyo anakuwa kiongozi wa kwanza wa Uingereza mwenye asili ya Kihindi, mwenye imani ya Kihindu na wa kwanza kutoka katika koloni la zamani la Uingereza. Akiwa na umri wa miaka 42, pia ndiye mkuu wa serikali mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Uingereza ya kisasa, baada ya kupanda ghafla katika siasa.

Anarithi nafasi ya Liz Truss, ambaye alihudumu kwa muda wa siku 49 uliovunja rekodi kufuatia upinzani juu ya mpango wake mkubwa wa kupunguza kodi. Liz Truss amemtakia waziri mkuu mpya "mafanikio" kwa majukumu aliyokabidhiwa, "kwa faida ya nchi yetu". Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Boris Johnson alituma "pongezi" zake kwa Waziri wake wa zamani wa Fedha Rishi Sunak kwa kuingia kwake madarakani katika siku hii ya "kihistoria".

"Maamuzi magumu" mbeleni

Baada ya kukutana na Charles III, Rishi Sunak alifika akiwa na uso wenye huzuni kidogo chini ya ushawishi wa maandamano mbele ya Downing Street kwa hotuba yake ya kwanza. Alikuwa peke yake bila mke na watoto wawili. 

Rishi Sunak ameahidi utulivu wa kiuchumi na zaidi ya yote kurejesha imani ya wapiga kura kupitia taaluma yake, uadilifu na uwajibikaji. “Makosa yalifanyika. Nilichaguliwa kuyarekebisha,” waziri mkuu mpya amesema. Bado alipongeza azimio la mtangulizi wake Liz Truss. Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Rishi Sunak pia ameonya kuhusu "maamuzi magumu" mbeleni. Rishi Sunak ameahidi kuanza kazi sasa.

Nchi yetu inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Ninataka kumpongeza mtangulizi wangu Liz Truss: alikuwa sahihi kutaka kuboresha ukuaji wa uchumi, na nilifurahia azimio lake la kufanya mambo yabadilike. Lakini alifanya makosa. Na nilichaguliwa, kama kiongozi wa chama changu na kama waziri mkuu, kuzirekebisha. Nitaweka utulivu wa kiuchumi na imani katika moyo wa hatua za serikali. Nitaileta nchi yetu pamoja. Serikali hii itadhihirisha uadilifu, weledi na uwajibikaji katika ngazi zote. Uaminifu unashinda na nitaomba muwe na uaminifu kwangu.

Kuhusu mzozo wa Ukraine, Rishi Sunak ameelezea uvamizi huo ulioanzishwa Februari kama "vita vya kutisha ambavyo lazima viishe kwa mafanikio" kwa Ukraine. Urusi ilikuwa imetangaza muda mfupi kabla ya hotuba ya Waziri Mkuu mpya kuwa "hakuna matumaini" ya kuboreka kwa uhusiano na Uingereza. Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amempongeza Rishi Sunak na kusema yuko tayari "kuendelea kuimarisha" uhusiano kati ya Ukraine na Uingereza.

Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, leo Jumanne ametuma "pongezi" zake kwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Rishi Sunak, katika ujumbe uliowekwa kwenye Twitter.

Hongera kwa RishiSunak ambaye anakuwa Waziri Mkuu wa Uingereza. Kwa pamoja, tutaendelea kufanya kazi ili kukabiliana na changamoto za sasa, ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine na athari zake mengi kwa Ulaya na kwa ulimwengu.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, amefanya vivyo hivyo, akitarajia kushirikiana "kama marafiki wa karibu" na Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.