Pata taarifa kuu
Jua Haki Zako

Kenya :Watoto wanaoishi na ulemavu vijijini wakosa mahitaji ya kimsingi

Imechapishwa:

Nchini Kenya Watoto walio na ulemavu nchini kenya hasa maeneo ya mashinani wanazidi kupitia changamoto si haba ukilinganisha na wenzao wa mijini.Hii ni kutokana na ufukara unaozidi kuongezeka mashinani.-Takwimu kutoka shirika la afya duniani zinaonyesha kuwa takriban watoto milioni 2.5 wanaishi na ulemavu nchini Kenya huku asilimia 72 ya watoto walemavu wanaishi mashinani na asilimia 27.4 wanaishi mijini.Mwandishi wetu, Victor Moturi, alitembelea kaunti ya Kisii na Nyamira

Wanaofunzi darasani nchini Kenya
Wanaofunzi darasani nchini Kenya © Victor Moturi
Matangazo ya kibiashara

Ni msimu wa mvua na  katika shule hii spesheli ya Mwata  iliyoko Kaunti ya Kisii nchini Kenya,wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kuongea wamekongamana darasani kupokea mafunzo;

Japo wanafunzi hawa wamo darasani,wamekosa vifaa muhimu vya mafunzo pamoja na chakula,Diana Metobo mmoja wa mwanafunzi  anasema wao wamekuwa wakipitia changamoto si haba..

‘’’Tuna  changamoto nyingi, tunakosa chakula, nguo, soksi, viatu, hatuna bweni zuri, maji hayapo. Nyumbani kwetu hatuna chakula na hata vitabu vya kusoma hakuna. Tunayo nyumba lakini ni ya zamani sana,’’Amesema Metobo.

 John Oigara  ni mwanafunzi mwingine asiye na uwezo wa kuongea ,Oigara anadokeza kuwa,.yeye pamoja na wanafunzi wengine, hutegemea msaada kutoka kwa majirani pamoja na wahisani wengine ,ili kujiendeleza kimasomo vile vile kupata mahitaji mengine.

‘’Wakati wageni walipokuja shuleni kwetu, walinunua chakula, blanketi, tangi la maji, sabuni, walituletea viatu, soksi na nguo.’’

 

Wanafunwi wakiwa darasani kaunti ya Kisii kenya
Wanafunwi wakiwa darasani kaunti ya Kisii kenya © Victor Moturi

 

Kilomita 40 kutoka mji wa kisii,shule ya msingi ya Riang’ombe DOK iliyoko Borabu ,kaunti ya Nyamira ni moja wapo ya shule zilizochaguliwa ili kutenga madarasa maalum kwa minajili ya watoto wanaoishi na ulemavu,lakini kulingana na mwalimu mkuu wa shule hii,George Onditi ,kwa muda sasa,wanafunzi hawajafika shuleni kwa sababu ya ukosefu wa waalimu pamoja na vifaa maalum vya masomo.

‘’,,,,Watoto walikuwa wengi,takriban ishiriki lakini kwa sababu nimekosa mwalimu,wengine wamefichwa,wengine hawakuji shuleni,wengine wakiingia wakiona mwalimu wao hayuko basi wanarudi kwa sababu sisi hawatuoni kama waalimu wao.Serikali tafadhali wanisaidie ,watusaidie kama jamii tuweze kupata waalimu,tuweze kupata vifaa,ndiposa tuwashughulikie haa watoto hawa watoto ambao ni walemavu,’’ Amesema George Onditi ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Riang’ombe

,,,,Kwa majina naitwa Stella Masaki,hili ni darasala la gredi 5,sasa wajua sisi hatujasomea taaluma hii,kwa hivyo tukiwachanganya hivi ,inatuchukuwa muda kuwafunza hawa badala ya kuwafunza wale ambao tumefunzwa jinsi ya kuwafundisha,kwa hivyo tunahitaji mwalimu ambaye atawashughulikia,wengine walichukuliwa na wazazi wao kwa sababu hatukuwa na uwezo wa kuwachunga,tukaona wale ambao wanaweza kuongea tukaona wabaki hapa tukae nao.

Idadi ya wanafunzi walio na ulemavu wanaojiunga na shule  vijijini ni chache mno ukilinganisha na wenzao wanaoishi mijini.

Hali hii imesababishwa na gharama ya juu ya vifaa vinavyohitajika kuwapa watoto hao mafunzo,ukosefu wa madarasa maalumu,na ukosefu wa usafiri .Agasa Maroko ni mwalimu maalum katika shule ya msingi magombo,kaunti ya Nyamira.

.’’.mimi nashughulikia wanafunzi ambao wana shida ya kiakili na wako wanafunzi kumi na watatu lakini kwa kijiji hiki kuna wale amabao hawajaingia shuleni kwa sababu hawana vifaa vya kuwaleta shuleni kama vile viti vya magurudumu.Hapa shuleni kuna mwingine akiona wenzake wanacheza nje anatoka darasani bila kuitisha ruhusa ,sasa mimi kama mwalimu ,lazima nitafute mbinu zote ambazo zitafanya huyo mtoto aingie darasani,na hata hawa walimu wengine kwa vile wana mapenzi kwa hao watoto,pia huwa wananisaidia sana’’Amedokeza mwalimu Maroko

 Wengi wa wanafunzi wanaoishi na ulemavu katika kaunti za kisii na nyamira ,hufichwa na wazazi ,hatua ambayo huwanyima haki zao za kimsingi pamoja huduma maalumu.

‘’kwa mfano unakuta shule zimejengwa ambazo watoto hawawezi pita kuingia darasani,vyoo vya kujisaidia hawawezi tumia na watoto wengine,sasa inabidi tunawafungia hawa watoto nyumbani,kama mimi ninaye mmoja aliyekuwa katika shule ya msingi ya Riang’ombe D.O.K,ikawa sasa hatangamani na watoto wengine kwa sababu ni mlemavu,na hawezi ingia darasani ,na lazima abebwe,hivyo ikabidi tumuweke nyumbani’’Amesema Shujaa Mathias Maina ambaye ni mzazi wa  mtoto anayeishi na Ulemavu.

 

Licha ya vizuizi hivi,Mashirika binafsi, kwa kushirikiana na utawala wa mitaa, wameanzisha mikakati na mipango ya kuongeza idadi ya wanafunzi wenye ulemavu wanaohudhuria shule nchini Kenya.Kama anavyoeleza Anthony Nyabera kutoka shirika la Progressive Africa, Ushirikiano huo una lengo la kutoa msaada muhimu kwa watoto wenye mahitaji maalum, kama vile vifaa vya masomo, sare za shule, viti vya magurudumu, na maelekezo ya kihisia.

,’’,Haswa tunawasaidia wale watoto walemavu,pia tunawasaidia wale wenye ni wagonjwa,pengine wanataka kuenda kliniki,tunawapeleka,kama Kijabe ,Kisii,na wakati mwengine madaktari wanawatembelea nyumbani,tulianza kuwafundisha watoto wale wako na shida ya uti wa mgongo,vile vile tukawalipia huduma ya NHIF na ndio huwa wanatumia kwa sasa,pia tunawasaidia na viti vya magurudumu ili viwasaidie kuenda shuleni,vile vile tunawapa vitanda maalum walio na shida za uti wa mgongo,wenye hawawezi kusimama au kutembea,pia kuna vile tunawasaidia’’Amedokeza Nyabera

Kupitia juhudi hizi, idadi kubwa ya watoto tayari wamenufaika. Zaidi ya watoto 3000 wamepokea msaada unaohitajika ili kuendelea na elimu yao, hivyo kuwawezesha  kuafikia malengo ya elimu.Esther Nyaribari,ni mkurugenzi mkuu katika shirika la Touching souls initiative nchini Kenya

‘’Mara ya kwanza tuligundua hawa watoto wako na changamoto za kupata chakula,na watoto hawawezi enda darasani na hawajakula,hivyo huwa tunatafuta wafadhili ambao husaidia hawa watoto kuwapa chakula kama vile mahindi maharagwe nakadhalika,halafu pia unapata watoto wamekuja shuleni wamevalia mavazi ya nyumbani,tunahakikisha tumewatafutia sare za shule angalau pia wafanane na wanafunzi wengine,pia kuna wale wanafunzi wenye umri mkubwa hasa wale walio na matatizo ya kiakili,pia hao tunawafikia manyumbani mwao na kuhakikisha maslahi yao yameshughulikiwa’’

 Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani, inakadiriwa kuwa watoto milioni 2.5 wanaishi na ulemavu nchini Kenya. Katika idadi hii, takribani asilimia 72 wanaishi katika maeneo ya vijijini, wakati asilimia 27.4 wanapatikana  mijini.Kwa mujibu wa Nyaribari, Takwimu hizi zinaonyesha hitaji la haraka la kushughulikia changamoto maalum zinazowakabili  watoto wenye ulemavu katika maeneo ya vijijini.

‘’Wito wangu kwa wazazi ni kuwa,wasifiche watoto na labda wasione wamepata watoto walemavu ni pigo wamepata,la hasha ,wawachukulie kama watoto wengine,wawatoe nje na wasiwafiche kwa sababu pia hao watoto wanahitaji masomo,wanahitaji matibabu na mambo mengine,kwa hivyo wawaweke wazi ndio sasa tuweze kuwasaidia kwa sababu wakiwaficha hatutaweza kujua kuna watoto wanahitaji msaada,’’Ameongeza Nyaribari

Huku idadi ya watoto wanaoishi na ulemavu ikizidi kuongezeka nchini Kenya,wazazi pamoja na mashirika ya kijamii ,wanaiomba serikali kuhakikisha uwepo wa vifaa vinavyohitajika kuwapa watoto hao masomo,kuongeza madarasa maalum vile vile kuajiri waalimu zaidi ili kupiga jeki masomo ya watoto wanaoishi na ulemavu.

Vipindi vingine
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.