Pata taarifa kuu
TANZANIA-UN-SUDAN

Tanzania yalaani tukio la kuuawa kwa wanajeshi wake wakulinda amani kwenye jimbo la Darfur

Serikali ya Tanzania imelaani tukio la kuuawa kwa wanajeshi wake saba wa kulinda amani nchini Sudan kwenye jimbo la Darfur kufuatia shambulio lililotekelezwa na waasi wanaoipinga Serikali ya Khartoum.  

Baadhi ya askari wa UNAMID wanaolinda amani kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan
Baadhi ya askari wa UNAMID wanaolinda amani kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa jeshi la wananchi wa Tanzania, JWTZ, kanali Kapambala Mgawe amesema jeshi la Tanzania limepokea taarifa za kuuawa kwa wanajeshi wake kwa masikitiko kwakuwa ni tukio la kwanza kubwa zaidi kuuawa kwa wanajeshi wa kulinda amani.

Kanali Mgawe ameongeza kuwa JWTZ limeunda timu ya uchunguzi kwenda nchini Sudan kwenye jimbo la Darfur kufanya uchunguzi wa tukio hilo kubaini hasa ni kwa vipi shambulio hilo lilitekelezwa.

Msemaji huyo akaongeza kuwa hivi sasa wanafanya mawasiliano na Umoja wa Mataifa UN kufanya utaratibu wa miili ya wanajeshi hao kurejeshwa nyumbani huku wale wengine zaidi ya kumi na tisa waliojeruhiwa wakiendelea kupatiwa matibabu.

Katika hatua nyingine rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao huko Darfur na kuitaka Serikali ya Sudan kufanyia uchunguzi tukio hilo.

Kauli ya rais Kikwete, ikapewa sauti na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon ambaye nae ameitaka Serikali ya Khartoum kufanya uchunguzi wa haraka kubaini ni kwa vipi waasi hao walipata mwanya na kuwashambulia wanajeshi wa kulinda amani.

Msemaji wa vikosi  vya UNAMID vilivyoko nchini Sudan kwenye jimbo la Darfur, Christopher Cymanick amesema tukio hilo lilitokea kwenye eneo la Khor Abeche kwenye mji wa Nyala ambao kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mapigano kati ya wanajeshi wa Serikali na waasi.

Hili ni tukio baya zaidi kuwahi kutekelezwa na waasi dhidi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wakulinda amani jimboni Darfur ambako kwa miaka mitano vikosi hivyo vimekuwa vikilinda amani kwenye jimbi hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.