Pata taarifa kuu
SYRIA

Shambulizi latikisa Damascus

Shambulizi kubwa la bomu  limetokea karibu na kambi ya kijeshi mjini Damascus nchini Syria inayopakana na hoteli ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yakisema makabiliano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali yameshuhudiwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Matangazo ya kibiashara

Runinga ya taifa ya Syria imeonesha picha za shambulizi hilo na kuripoti kuwa watu watatu wamejeruhiwa lakini waangalizi wa Umoja wa Mataifa hawakuwa miongoni mwao.

Mapigano  yanayoendelea nchini Syria kati ya waasi na wanajeshi wa serikali yamefika katika jiji la Damascus katika siku kadhaa zilizopita, huku lengo la shambulizi la Jumatano likiwa halijulikani.

Mwezi uliopita,shambulizi lingine la bomu lilitokea katika ofisi za usalama wa kitaifa na kusababisha mauji ya watu watatu washirika wa karibu wa rais Bashar Al Assad akiwemo waziri wa Ulinzi.

Kwingineko,mkutano wa dharura wa mataifa 57 ya muungano wa Kiislamu umeingia katika siku yake ya pili mjini Jeddah nchini Saudi Arabia, kujadili mzozo wa Syria.

Lengo la mkutano huo ni kujadili machafuko nchini Syria na kukashifu machafuko yanayoendelea na pia kutangaza kuisimamisha  Syria kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.

Ikiwa Syria itasimamishwa uanachama katika muungano huo, itakuwa ni njiamojawapo ya kushinikiza uongozi wa rais Bashar Al Assad kuondoka uongozini.

Kikao hicho kinaongozwa na Mfalme wa Saudi Arabia Abdullah ambaye alipendekeza kusimamishwa kwa uanachama wa Syria katika muungano huo, mkutano ambao pia unahudhuriwa na rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, ambaye anasalia kuwa mshirika wa karibu wa rais Assad.

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa rais Assad, imeendelea kuyalaumu mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kwa kuchochea machafuko nchini Syria.

Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov amesema, Urusi haitakubali mataifa hayo kuendelea kuunga mkono waasi na  inatoa wito kwa mataifa hayo ya Magharibi kuzingatia  makubaliano waliyotia saini mwezi Juni mjini Geneva Swizerland kutatua machafuko ya  Syria kisiasa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika linalohusika na maswala ya kibinadamu Valarie Amos yupo mjini Damascus ambapo ametoa wito kwa wapiganaji na wanajeshi wa serikali kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia waathiriwa wa machafuko hayo.

Katika hatua nyingine, Marekani inaituhumu Iran kuwa inawapa mafunzo waasi wa Syria kuendelea kupambana na wapiganaji wa upinzani nchini humo.

Machafuko nchini Syria yameingia katika mwezi wa 17 ambapo maelfu ya watu wameuawa na wengine kukimbia makwao.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.