Pata taarifa kuu
TANZANIA-CUF

Sintofahamu kubwa ya kiuongozi ndani ya chama cha upinzani Tanzania, CUF

Mgogoro mkubwa wa kiuongozi unakikabili kilichowahi kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CUF, ambapo juma hili baraza kuu la chama hicho lililokutana visiwani Zanzibar, limeridhia kumfukuza uanachama rasmi aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Ibrahim Lipumba.

Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amefukuzwa rasmi ndani ya chama chake.
Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amefukuzwa rasmi ndani ya chama chake. https://ismailjussa.files.wordpress.com
Matangazo ya kibiashara

Akisoma maazimio yaliyofikiwa baada ya kikao hicho, mwenyekiti aliyeongoza Katani Ahmad, aliwaambia wanahabari kuwa, baada ya kupitia hoja sita zilizowasilishwa na katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, baraza kuu la chama liliridhia kwa kauli moja kumfuta uanachama.

Miongoni mwa hoja zilizopelekea kuvuliwa uanachama wake ni pamoja na tukio la mwishoni mwa juma lililopita, ambapo Lipumba akiwa ameambatana na wafuasi wake, walivamia makao makuu ya chama hicho yaliyoko Tanzania bara eneo la Buguruni na kufanya fujo.

Akiwa ofisi hapo Lipumba alidai kuwa yeye bado anatambua ni mwenyekiti wa chama hicho taifa, kwakuwa hakukuwa na kikao chochote cha halali kilichoketi kuridhia barua yake ya kujiuzulu zaidi ya kile cha Agosti mbili ambacho kilipiga kura kukataa kurejeshwa kwenye nafasi yake.

Kwenye hoja hizo sita zilizowasilishwa na katibu mkuu wa chama, baraza hilo lilieleza kusikitishwa na hatua ya kiongozi huyo kukataa kuitikia wito wa barua aliyoandikiwa akitakiwa kufika visiwani Zanzibar Jumanne ya wiki hii kwaajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Ibrahim Lipumba (kushoto) aliyekuwa mwenyekiti taifa wa CUF akiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Seif Shariff Hamad, hapa ni wakati hajajiuzulu nafasi yake ya uenyekiti
Ibrahim Lipumba (kushoto) aliyekuwa mwenyekiti taifa wa CUF akiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Seif Shariff Hamad, hapa ni wakati hajajiuzulu nafasi yake ya uenyekiti DR

Akizungumza na idhaa hii, Ibrahim Lipumba alisisitiza kuwa yeye bado ni mwenyekiti wa chama cha CUF na hatambui kikao chochote kilichoketi visiwani Zanzibar kumjadili kwakuwa hakikuwa na uhalali wowote.

Mwishoni mwa juma pia msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, ambaye pia ni mlezi wa vyama hivyo, aliiandikia barua CUF, akiwataka kuheshimu katiba yao na kutoa mapendekezo ya kumrejesha kwenye nafasi yake Ibrahim Lipumba, barua ambayo baraza kuu la CUF limesema halitaishughulikia na kwamba msajili hana mamlaka ya kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana wa mwezi October, Ibrahim Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi ya uenyekiti taifa wa chama hicho, kwa kile alichodai wakati huo, kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho, akidai watu wasiofaa waliingizwa kuwania urais.

Hata hivyo mapema mwaka huu, Lipumba aliandika tena barua kwa katibu mkuu wa chama akiomba kurejeshwa kwenye nafasi yake, kwa madai kuwa aliombwa kufanya hivyo na wanachama na hata hivyo hakukuwa na kikao halali kilichoketi kuridhia kujiuzulu kwake.

Haya yanajiri wakati huu chama hicho kikikataa kutambua matokeo ya urais visiwani Zanzibar, kufuatia uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi March mwaka huu baada ya ule wa mwaka jana kufutwa kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa utangazwaji wa matokeo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.