Pata taarifa kuu
KENYA

Mawakili nchini Kenya wagoma baada ya mwenzao kuuawa

Mawakili nchini Kenya wanaaza mgomo wa wiki moja kuanzia hivi leo kulaani kuuawa kwa mwenzao Willie Kimani, mteja wake na dereva wa Taxi wiki iliyopita katika Kaunti ya Machakos.

Waandamanaji wa mawakili nchini Kenya
Waandamanaji wa mawakili nchini Kenya mary@kenyans.co.ke
Matangazo ya kibiashara

Muungano wa Mahakimu na Majaji nchini humo umeunga mkono mgomo huo na kusema mauaji dhidi ya wakili huyo yalilenga kuwatisha mawikili.

Pamoja na mgomo huo, kuna maandamano ya kitaifa ya mawakili hao kushinikiza serikali kuunda Tume maalum kuchunguza mauaji ya wakili huyo wa haki za binadamu.

Jijini Nairobi, mamia ya Mawakili, wanaharakati wa haki za binadamu na madereva wa magari ya Taxi walikusanyika katika bustani ya Uhuru Park kuanzia asubuhi, kabla ya kuelekea kwenye makao makuu ya jeshi la Polisi na Ofisi ya rais kushinikiza kujiuzulu kwa Mkuu na Polisi na Waziri wa Mambo ya ndani Joseph Nkaissery.

Inspekta Mkuu wa polisi Joseph Boinett wiki iliyopita alitangaza kuwa maafisa watatu wa polisi wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo wamekamatwa.

Washukiwa hao tayari wamefikishwa Mahamakani na kufunguliwa mashtaka ya mauaji na wamezuiliwa kwa wiki mbilli ili kiongozi wa mashtaka kumaliza uchunguzi wake.

Seneta wa Mombasa Omar Hassan Omar ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu, amemshtumu Mkuu wa jeshi la polisi na Waziri wa Mambo ya ndani kwa kushindwa kukomesha mauaji kama haya.

Mbali na mauaji haya, wanaharakati hao wanataka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu hatima ya mamia ya vijana hasa kutokea Pwani ya nchi hiyo ambao wametoweka na hawajulikani walipo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.