Pata taarifa kuu
TANZANIA-SIASA

Upinzani Tanzania: Hatutakubali kufungwa mdomo

Wabunge wa upinzani nchini Tanzania, wameendelea kutoka nje ya ukumbi wa bunge la Jamhuri ya Muungano wakati vikao vikiendelea, ikiwa ni muendelezo wa kupinga mwenendo wa bunge na namna naibu spika anavyoendesha vikao. 

James Mbatia kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, akizungumza nje ya Bunge baada ya kutoka, 20 Juni 2016
James Mbatia kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, akizungumza nje ya Bunge baada ya kutoka, 20 Juni 2016 RFI
Matangazo ya kibiashara

Jumatatu ya wiki hii, wabunge wa upinzani walitoka nje ya ukumbi wa bunge dakika chache baada ya naibu spika kufungua kikao hicho kwa sala.

Wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Vunjo, James Mbatia, walianza kutoka kwa makundi wakati kipindi cha maswali na majibu kimeanza, huku safari hii wakiwa wamefunika midomo yao kwa kitambaa cheupe kuashiria kufungwa mdomo na Bunge.

Ni majuma kadhaa sasa wabunge wa upinzani wameendelea kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, kwa kile wanachosema kuwa naibu spika wa bunge, Dr. Tulia Ackison wamekuwa akipendelea upande mmoja wa wabunge wa chama tawala.

Mwenyekiti mwenza wa muungano wa vyama vya upinzani UKAWA, James Mbatia, amesema kuwa hatua yao ya leo kuamua kutoka nje ya bunge wakiwa wamevalia vitambaa kufunika midomo yao, ni ishara tosha ya kuendelea kuonesha kutoridhishwa na namna vikao hivyo vinavyoendeshwa.

Wabunge wa vyama vya upinzani walipokuwa wakianza kutoka Bungeni, Jumatatu, June 20, 2016.
Wabunge wa vyama vya upinzani walipokuwa wakianza kutoka Bungeni, Jumatatu, June 20, 2016. RFI

Mbatia ameongeza kuwa hatua ya Serikali na uongozi wa bunge kuamua kukacha wito wao wa kufanyika kwa mazungumzo ili kufikia maridhiano, ni isahara ya wazi ya kile alichosema kuminywa kwa uhuru wa wabunge kutoamaoni Bungeni.

Upinzani unasema ni majuma kadhaa sasa toka kuanza kwa mjadala wa bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2016/2017, wao wamekuwa wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge, kupinga kitendo kinachofanywa na naibu spika kupendelea upinzani pamoja na kuruhusu baadhi ya wabunge wa chama tawala kumdhihaki kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni.

Viongozi wa upinzani wanasema kamwe hawatakubali kushirikiana na Serikali kwenye shughuli zozote hata zile za nje ya Bunge, kwa kuwa wanaamini mawazo yao kwenye bajeti ya mwaka huu, yalikuwa muhimu na Serikali ilipaswa kuingilia kati baada ya kukosekana kwa maridhiano ndani ya Bunge.

Mvutano huu ulianza wakati ilipozuiliwa kusomwa Bungeni hotuba ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu wizara ya mambo ya ndani, na kisha baadae kuibuka kwa sakata la kijinsia ambapo Mbunge mmoja wa chama tawala aliwakashifu wabunge wanawake wa upinzani na kusababisha watoke nje kususia kikao baada ya spika kutochukua hatua yoyote.

Hata hivyo ofisi ya Bunge pamoja na naibu spika mwenyewe, mara kadhaa alilitolea ufafanuzi suala hili, ambapo alisema wabunge hao kutoka nje ni haki yao kwakuwa hawakulazimishwa kufanya hivyo, na kuongeza kuwa hata posho za vikao hawatapewa kwasababu hawahudhurii vikao vinavuoendelea mjini Dodoma.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.