DR Congo: Serikali kufuatilia kesi dhidi ya mwanahabari Stanis Bujakera
Nairobi – Serikali ya DRC, kupitia waziri wake wa mawasiliano, Patrick Muyaya, imesema inafuatailia kwa karibu kesi dhidi ya mwanahabari Stanis Bujakera, aliyakamatwa kwa tuhuma za kuandika habari za uongo kuhusu kifo cha waziri wa zamani Cherubin Okende.
Imechapishwa:
Stanis Bujakera anadaiwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu ripoti iliyo chapiswa na Jeune Afrique ikihusisha ujasusi wa kijeshi katika mauaji ya aliyekuwa waziri wa zamani Chérubin Okende.
Baada ya kukamatwa kwake katika uwanja wa ndege wa Ndjili wakati akitarajia kwenda mjini Lubumbashi, simu zake na kompyuta zilichukuliwa na vyombo vya usalama.
Mwanahabari huyo ametakiwa na idara ya ujasusi kuweka wazi waliompa taarifa hiyo.
Waandishi wa habari nchini DRC wanasema wameghadhabidshwa na kukamatwa kwa mwenzao. Kwa mujibu wa EDMOND IZUBA, msemaji wa muungano wa waandishi wa habari wa Kongo amesema, taarifa iliyochapishwa na Jeune Afrique haina saini yake.
“Ikiwa serikali iliona ripoti hio ambayo ilichapiswa na jeune Afrique ni ya uongo, basi wangefuata kipengele cha 104 kuhusu sheria ya uhuru wa vyombo vya habari inayowapa nafasi watupilie mbali tuhuma ya ripoti hio.”alieleza Edmond Izuba.
Edmond Izuba- Msemaji wa Muungano wa wanahabari nchini DRC
Shirika la kutetea haki za binadamu la voix des sans voix limeomba vyombo vya sheria kutoa mwanga kuhusu mauaji ya waziri huyo wa zamani ambaye pia alikuwa mtu wa karibu wa mwanasiasa wa upinzani MOISE KATUMBI.
Ronsard MANKETA ni katibu mtendaji wa shirika hilo.
“Ingekuwa vizuri aachiliwe huru kuliko kupelekwa katika gereza la Makala, mahakama ya Kongo inatakiwa kuleta mwanga kuhusu mauaji ya mbunge Chérubin Okende, kuliko kumshambulia mwandishi wa habari ambaye alifanya kazi yake.” alisema Ronsard Manketa.
Ronsard Manketa
Kwa upande wake waziri wa habari aliahidi kufuatilia kwa karibu suala hili. “Hili ni swali ambalo liko chini ya mamlaka ya mahakama” alisema Patrick Muyaya.
Balozi kadhaa zimeelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya mwanahabari huyo wakati huu ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika tarehe 20 Desemba.
Freddy Tendilonge/ Kinshasa/RFI Kiswahili