Pata taarifa kuu

Ziara ya Antony Blinken yaibua matarajio mengi nchini DRC

Antony Blinken anawasili Kinshasa Jumanne hii kwa ziara ya siku mbili sawa na saa 48. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani atakutana na Rais Félix Tshisekedi na viongozi wengine wachache wa kisiasa wa DRC. 

Antony Blinken na Félix Tshisekedi wakati wa mkutano kando ya Mkutano Mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa, mnamo Septemba 2021.
Antony Blinken na Félix Tshisekedi wakati wa mkutano kando ya Mkutano Mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa, mnamo Septemba 2021. AFP - EDUARDO MUNOZ
Matangazo ya kibiashara

 

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari katika Ofisi ya rais wa Jamhuri na Wizara ya Mambo ya Nje, suala la usalama litatawala  mazungumzo kati ya mamlaka ya Kongo na kiongozi huyo wa Marekani. 

DRC inatarajia mengi kutoka kwa Marekani, hasa kuhusu kundi la waasi la M23 na mivutano kati ya Kinshasa na Kigali.

Kwa kutegemea hasa ripoti ya hivi majuzi ya kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaosema wana uthibitisho wa uungaji mkono wa jeshi la Rwanda kwa kundi la waasi la M23, mamlaka ya DRC inatarajia kutoka kwa Antony Blinken kuilaani Rwanda waziwazi, anaeleza mwandishi wetu mjini Kinshasa, Patient Ligodi.

Kinshasa inabaini kwamba kundi hili lenye silaha linajizatiti baada ya Kigali kulipa msaada wa kijeshi na silaha na kwa hiyo inamtaka Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuweka shinikizo zaidi kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame. Kulingana na wasaidizi wa Félix Tshisekedi, mamlaka ya DRC pia inatumai kwamba Marekani italiweka kundi la M23 kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi kama walivyofanya Machi 2021 kwa kundi la waasi wa Uganda ADF.

Kabla ya kuondoka Afrika Kusini, Antony Blinken pia alielezea "wasiwasi" wake kuhusu hili na kusema anahofia kuwa "hali itazidi kuwa mbaya". Alihakikisha kwamba Washington "itajaribu kupunguza mvutano na vurugu" kupitia diplomasia, akitumai kusaidia DRC na Rwanda "kutafutia suluhu tofauti zao".

Lakini sio serikali pekee inayotarajia msimamo thabiti kutoka kwa Marekani kwenye suala hii. Mashirika ya kiraia pia. Floribert Anzuluni, mratibu wa Filimbi, vuguvugu linalounga mkono demokrasia, anamuomba waziri wa mambo ya nje wa Marekani "kuweka shinikizo kwa Kigali" na washirika wengine wa kimataifa "kwa Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake katika ardhi ya DRC".

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.