Pata taarifa kuu

Rais mpya wa mpito Jamhuri ya Afrika ya Kati apania kuboresha maridhiano kati ya wananchi wake

Vifijo nderemeo na shamrashamra za kila aina zimeendelea kushuhudiwa usiku kucha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kufuatia hapo jana bunge la mpito la nchi hiyo kumeteua aliyekuwa Meya wa jiji la Bangui, Catherine Samba-Panza kuwa rais wa mpito. Panza ambaye anakuwa mwanamke wa tatu barani Afrika kuteuliwa kushika nafasi ya urais aliwashinda wagombea wengine saba ambao nao walikuwa wakiwania nafasi hiyo ambapo sasa rais huyo anakabiliwa na changamoto ya kumaliza machafuko nchini humo.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Mara baada ya jina lake kutangazwa kama mshindi kwenye uchaguzi, shamrashmra zilianzia bungeni kabla ya mji wa bangui kulipuka kwa furaha ambapo wananchi wengi wameonesha kuunga mkono uteuzi wake.

Kwenye Hotuba yake ya awali kufuatia uteuzi wake, rais Panza anasema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha anasuru maisha ya raia wake ambao tayari wako kwenye hali mbaya.

“Haraka iwezekanavyo, kipaumbele namba moja ni kusitisha mateso ya wananchi wetu kwa kuwaletea msaada wananohitaji na kuandaa mazingira ya kurejelea makazi yao.

Kurejesha mamlaka ya serikali na usalama nchini kote, na kuwaunganisha wananchi wote kwa njia ya maridhiano ili kuanza mchakato wa maendeleo katika sekta binafsi na ya umma”, amesema rais Panza.

Kuhusu masuala ya usalama na kuleta umoja wa kitaifa nchini humo, rais Panza ametoa wito kwa makundi ya Seleka na Anti-Balaka kuweka silha chini na kuhubiri amani kwenye taifa hilo.

“Mimi ni rais wa wananchi wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati bila ya ubaguzi. Kwa hiyo, natoa wito wangu kwa mmoja wenu kuunga mkono jukumu la ujenzi wa nchi yetu.

Nawaomba wanangu Anti-Balaka mnaonisikia, mnidhihirishie uungwaji mkono wenu kwa uteuzi wangu kwa njia ya kuweka silaha chini”, amesema rais Panza.

Hata hivyo uteuzi wake umeungwa mkono hata na makundi yanayokinzana nchini humo. Kiongozi wa muungano wa Seleka, Jenerali Mahamat Ousmane amesema wameridhika kwa uteuzi huo wa rais mpya wa mpito.

“Binafsi nimeridhika na kwa niaba ya muungano wote wa Seleka hata wananchi wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Muungano wa seleka, wapiganaji wake pamoja na wanansiasa wake tutamuunga mkono rais mpya, ili kuimarisha amani, usalama na maendeleo ya nchi yetu. Wajibu wetu ni kumuunga mkono rais wetu hadi mwisho wa muda wake”, amesema Ousmane.

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine zaidi ya 400,000 kuyahama makaazi yao.

Jumuiya ya kimataifa pia imepongeza uteuzi wa catherine Samba-Panza ambaye nchini mwake amepata umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake wa kuongoza kama meya na namna ambavyo amekuwa akiwajali wananchi wote bila kubagua.

Hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa unasema kuwa mashirika yake yanakabiliwa na uhaba wa chakula cha msaada nchini jamhuri ya Afrika ya kati wakati huu idadi ya watu wanaokimbia machafuko nchini humo ikiongezeka kufuatia mapigano yanayoendelea kushuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo.

Shirika la mpango wa Chakula duniani, WFP hapo jana limesema kuwa wafanyakazi wake walishindwa kuingia nchini humo kupitia mpaka wa Cameroon kuhofia msafara wake kushambuliwa na makundi ya watu ambao wamekuwa wakiteka magari yanayobeba chakula cha msaada.

Katika hatua nyingine mshauri wa masuala ya kuzuia mauaji ya halaiki kwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa UN, Ban Ki Moon, Adama Dieng amesisitiza umoja huo kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya usalama inarejea nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza misaada zaidi kwa wananchi.

Kauli ya Dieng inakuja wakati huu taifa la Jamhuri ya Afrika ya kati likimpata kiongozi wake wa mpito, Catherine Samba-Panza ambaye anakuwa ni mwanamke wa tatu barani Afrika kushika wadhifa wa urais kwenye taifa ambalo linakabiliwa na changamoto ya mauji ya wenyewe kwa wenyewe.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.