Pata taarifa kuu
AFRIKA KUSINI

Jengo laporomoka nchini Afrika Kusini na kusababisha kifo cha mtu mmoja

Mamia ya waokoaji wamefanya kazi usiku kucha wakitafuta manusura waliofukiwa na kifusi baada ya jengo la maduka lililokuwa katika ujenzi kuanguka karibu na mji wa Durban nchini Afrika Kusini jana Jumanne, imethibitishwa kuwa mpaka sasa mtu mmoja amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa. Msemaji wa polisi Mandy Govender amethibitisha kifo cha mtu huyo na kusema watu wengine 26 wamepatikana wakiwa hai katika mabaki ya kifusi baada ya paa la maduka kuporomoka.

AP Photo
Matangazo ya kibiashara

Aidha Govender amesisitiza kuwa wengi wa walionaswa ndani ya jengo hilo ni wafanyakazi waliokuwa wakiendelea na ujenzi, na inahofiwa kuwa takribani watu 50 bado wamekwama ndani ya kifusi.

Watoa huduma za dharura toka katika kampuni ya ER24 wanasema majeruhi walio katika hali mbaya wamekimbizwa hospitalini kwa ajili ya huduma zaidi na wengine wanaendelea kupatiwa huduma ya kwanza.

Hata hivyo juhudi za uokoaji zimesitishwa kwa muda na zoezi hilo litaendelea baada ya kuondoa baadhi ya matofali, mashine kubwa imepelekwa katika eneo hilo ili kuondoa matofali hayo.

Saa 19 baada ya uokoaji kuanza matumaini ya kuwapata watu wengine wakiwa hai yameanza kupotea, dalili za kuwapata manusura wengine zimezidi kupungua kadri muda unavyozidi kusonga mbele.

Chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo bado hakijabainika, ingawa imefahamika kuwa kampuni ya ujenzi iliyokuwa inaendesha shughuli zake hapo mwezi uliopita ilipewa amri ya mahakama ya kusitisha ujenzi huo.

Msemaji wa jimbo, Thulani Zwane amesema uchunguzi wa kina unaedeshwa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

 

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.