Pata taarifa kuu
TANZANIA-EAC

Kikwete: Tanzania si chanzo cha kukwamisha maendeleo katika jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki EAC

Nchi ya Tanzania imeahidi kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu katika jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na kukanusha kuwa yenyewe imekuwa chanzo cha kukwamisha maendeleo ya Jumuiya hiyo. Akilihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alhamisi hii mjini Dodoma, Rais wa nchi hiyo Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza kuchukizwa kwake na namna ambavyo baadhi ya nchi wanachama wanataka kuharakisha shirikisho la Afrika Mashariki hata kabla ya kufuata hatua muhimu za kuanzishwa kwake.

http://michuzi-matukio.blogspot.com
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Rais Kikwete inatolewa wakati huu ambapo kumekuwa na mgawanyiko wa dhahiri kwenye misimamo ya viongozi wa jumuiya kuhusu masuala kadhaa ikiwemo miundo mbinu na utiwaji saini wa mikataba inayohusisha jumuiya nzima.

Tanzania imeweka wazi kuwa haina mpango wa kujitoa EAC kwani haijaenda kunyume na mkataba wa jumuiya hiyo na imekuwa ikitumia gharama kubwa kuhakikisha jumuiya hiyo inaimarika.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, hata hivyo Tanzania na Burundi ndio zimeonekana kutengwa katika vikao vya hivi karibuni.

Kenya, Uganda na Rwanda zimeshafanya vikao vitatu Mombasa Kenya, Kampala Uganda na Kigali Rwanda, na viongozi wa nchi hizo waliamua mambo nane ya msingi ambayo yanaonekana kudhihiridha wazi tofauti za misimamo ndani ya jumuiya.

Rais Kikwete alisema wazi kuwa nchi hizo zimekiuka Mkataba wa EAC katika mambo manne kati ya mambo nane waliyoyajadili katika vikao vyao walivyovifanya.

Nchi ya Tanzania imekuwa na msimamo wa kupinga kuharakisha uundwaji wa shirikisho, hatua ambao Rais Kikwete anasema inapaswa kwenda sambamba hatua kwa hatua na wala si kukurupuka.

Tanzania inataka hatua zifuatwe kwa kuanza na uundwaji wa umoja wa forodha, soko la pamoja, umoja wa fedha na baadaye lifuate shirikisho la kisiasa, ambalo litafikiwa baada ya kura ya maoni ya wananchi wa nchi wanachama.
 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.