Pata taarifa kuu
SYRIA

Syria yasema Makundi ya Kigaidi kutoka Mataifa 38 ndiyo yamekuwa yakitekeleza mauaji ya wananchi na wanajeshi

Serikali ya Syria imekuwa mbogo na kutoa lawama zake kwa Mataifa thelathini na nane ambayo yamechangia kupeleka Magaidi wake katika ardhi ya Damascus na kuendesha vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha vifo vya wanajeshi wa Serikali pamoja na wananchi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Al Muallem akihutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Al Muallem akihutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA
Matangazo ya kibiashara

Syria imesema Taifa hilo limekuwa sehemu ya magaidi kutoka mataifa zaidi ya thelathini na nane na wamekuwa wakiendesha vitendo vya ugaidi tangu wamefanya uvamizi wao uliokaliwa kimya na jumuiya ya Kimataifa na kuchangia kuleta madhara makubwa kwa wananchi wao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Muallem ndiye ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Sitini na Nane wa Umoja wa Mataifa UNGA na kusema wakati umefika wa kuhakikisha magaidi hao wanatokomezwa na kufukuzwa nnje ya mipaka ya Damascus.

Muallem alikwenda mbali zaidi na kufananisha uvamizi uliofanywa na magaidi hao kuwa sawa kabisa na shambulizi la kigaidi lililotekelezwa nchini Marekani kwenye Jiji la New York tarehe 11 mwezi Septemba na kuchangia vifo vya raia wasio na hatia.

Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya nje ameweka bayana nchi yake mmekuwa mstari wa mbele kupambana na Makundi hayo ya Kigaidi lakini wamekuwa wakigonga mwamba kutokana na kuendelea kupatiwa ufadhili.

Muallem amesema kitendo cha kuendelea kuyapa ufadhili makundi hayo ya Kigaidi kunakofanywa na Uturuki, Saudi Arabia na Qatar ndiko kunafanya kazi ya kuwaangamiza kuendelea kuwa ngumu kwani wamekuwa na silaha za kuendeleza mashambulizi.

Syria imeweka bayana hata mazungumzo ya Geneva yanayosimamiwa na Urusi na Marekani yanaweza yasilete mabadiliko yoyote iwapo mataifa hayo yataendelea kuwafadhili kwa silaha wapinzani wanaopata usaidizi kutoka kwa Makundi ya Kigaidi.

Muallem amesisitiza Makundi hayo ya Kigaidi yamekuwa yakifanya vitendo vya mauaji ya kinyama ikiwemo kuwaua wafuasi wa Rais Bashar Al Assad na kisha kuchukua baadhi ya viungo na kuwapelekea ndugu zao.

Katika hatua nyingine Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa UN wameondoka nchini Syria baada ya kumaliza kazi yao ya kufanya uchunguzi kubaini upande gani umekuwa ukutumia silaha za kemikali.

Wachunguzi hao walirejea tena Damascus baada ya kutoa ripoti iliyothibitsha kumekuwa na matumizi ya silaha za kemikali zenye sumu ya sarin nchini Syria kwenye mashambulizi yaliyofanyika tarehe 21 mwezi Agosti.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.