Pata taarifa kuu
DRC-RWANDA-MAREKANI

Marekani yaitaka Rwanda kuacha mara moja kulifadhili Kundi la Waasi la M23 na kuondoa Wanajeshi wake Mashariki mwa DR Congo

Serikali ya Marekani imetoa karipio kali kwa Rwanda kuacha mara moja kuwafadhili Waasi wa Kundi la M23 linalopambana na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC na kuwataka kuondoa wanajeshi wao waliopo katika eneo la Mashariki mwa DRC. Serikali wa Washington imesema hili ni tamko kali ambalo halina masihara hata kidogo kwa kuwa wanaushahidi wa kutosha kuonesha Jeshi la Rwanda limeendelea kuwepo mashariki mwa DRC na kuwasaidia Wapiganaji wa Kundi la M23 kuzorotesha usalama.

Kikosi cha Wanajeshi wa Rwanda kilichokuwepo Mashariki mwa DR Congo wakati kinaondoka
Kikosi cha Wanajeshi wa Rwanda kilichokuwepo Mashariki mwa DR Congo wakati kinaondoka
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Jen Psaki amewaambia wanahabari Rwanda inatakiwa kuacha mara moja kuendelea kulifadhili Kundi la Waasi la M23 na kisha kuondoa wanajeshi wake wote ili kutimiza ahadi walizoziweka.

Psaki ameweka bayana wameshakusanya ushahidi wa kutosha kuthibitisha Rwanda imeendelea kutoa ufadhili kwa Wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23 ambalo limeendelea kupambana na Jeshi la FARDC wakitaka kuuteka Mji wa Goma.

Msemaji huyo wa Mambo ya Nje amesema ushahidi wao wameukusanya kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzungumza na Maofisa wa Rwanda ambao wamekiri wanajeshi wao wapo Mashariki mwa DRC kuwasaidia wapiganaji wa Kundi la M23.

Tamko la Marekani limekuja baada ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch kuanika ushahidi wake ya kwamba Serikali ya Rwanda imeendelea kutoa ufadhili kwa Kundi la Waasi la M23.

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch imepingwa vikali na Serikali ya Kigali ikisema imejaa uzushi na uongo kwani kuna sehemu inaeleza Rwanda imeshawahi kupeleka wanajeshi wake kulinda amani nchini Somalia kitu ambacho hawajawahi kukifanya.

Licha ya Rwanda kuishutumu ripoti hiyo lakini imeonesha namna ambavyo Rwanda imekuwa ikituma wanajeshi wake ndani ya Kundi la Waasi la M23 ili kuliimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya Jeshi la FARDC.

Ripoti ya Shirika la Human Rights Watch inaonesha pia namna ambavyo Kundi la Waasi la M23 lililowaua watu 44 na kisha kuwabaka wanawake na wasichana wapatao 61 Mashariki mwa DRC tangu mwezi Machi mwaka 2013.

Mkurugenzi wa Shirika la Human Rights Watch kwa Afrika Daniel Bekele amesema ni Rwanda pekee ambayo imekuwa tayari kuruhusu mipaka yake kutumika kwa Waasi la Kundi la M23 kuendelea kufanya vitendo vya kihalifu na wao kunyamaza kimya.

Bekele ameendelea kubainisha msaada wa Rwanda kwa Kundi la Waasi la M23 umekuwa chachu ya kufanyika kwa mauaji, ubakaji na ukatili mwingine dhidi ya binadamu wanaoishi Mashariki mwa DRC.

Rwanda imekuwa rafiki mkubwa wa Marekani lakini mwaka jana iliingia matatani na kukosa msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola 200,000 kutokana na kutuhumiwa kulifadhili Kundi la Waasi la M23.

Katika hatua nyingine Jeshi la Serikali FARDC limeendelea kukabiliana na Wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23 ambao wamekuwa mstari wa mbele kutaka kuuteka Mji wa Goma.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.