Pata taarifa kuu
SYRIA-UFARANSA

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Syria anatarajiwa kukutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande ili kuomba msaada wa Kijeshi

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Syria Ahmad Jarba anatarajiwa kukutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande baadaye hii leo akiwa na lengo lakuendelea kuisisitiza nchi hiyo kutekeleza ombi lao la kupatiwa msaada wa kijeshi ili kukabiliana na Majeshi ya Serikali ya Rais Bashar Al Assad.

Kiongozi Mkuu wa Baraza la Upinzani nchini Syria SNC Ahmad Jarba akihutubia waandishi wa habari
Kiongozi Mkuu wa Baraza la Upinzani nchini Syria SNC Ahmad Jarba akihutubia waandishi wa habari
Matangazo ya kibiashara

Jarba amewaambia wanahabari lengo lao ni kupata msaada zaidi wa kijeshi ambao utawasaidia kushinda katika vita vinavyoendelea kati yao na Jeshi la Serikali linalomtii Rais Assad na ombi hilo ameshaliwasilisha katika Kamati ya Bunge inayoshughulikia Mambo ya Nje.

Kiongozi huyo wa Upinzani nchini Syria ameongeza licha ya kuhitaji msaada huo wa kijeshi lakini wanataka kupata uungwaji mkono kwenye masuala ya siasa, diplomasia, misaada ya kibinadamu na masuala mengi muhimu ambayo yatawafanya watambulike kama wawakilishi kamili wa wananchi.

Jarba ametembelea Ufaransa kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa kushika wadhifa wa kuongoza Upinzani tarehe 6 ya mwezi Julai na mwenyewe amekiri kupata mwaliko kutoka kwa Rais Hollande unadhihirisha lengo la Serikali ya Paris katika kulinda maslahi ya wananchi wa Syria.

Kiongozi huyo wa Baraza la Upinzani nchini Syria SNC akishakutana na Rais Hollande anatarajiwa kuelekea Jijini New York kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa UN ambao pamoja na mambo mengine unatarajiwa kujadili mustakabali wa baadaye wa Taifa hilo.

Uingereza imeshaweka wazi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC wakiwepo Urusi na China watakutana siku ya Ijumaa kwa mara ya kwanza na Viongozi wa Baraza la Upinzani nchini Syria SNC.

Mapema Mkuu wa Majeshi ya Baraza hilo la Upinzani Jenerali Selim Idriss aliweka bayana wameendelea kufanya kazi pamoja na mataifa rafiki kutoka Barani Ulaya na Marekani lengo likiwa ni kuwapa mbinu zaidi na msaada wa kijeshi ili kuhakikisha wanaung'oa utawala uliopo madarakani.

Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa UN umeingiwa na hofu huenda uchunguzi wa kubaini uwepo wa matumizi ya silaha za kemikali usifanikiwe baada ya Wapiganaji wa Upinzani kufanikiwa kuuteka Mji wa Khan Al Assal uliokuwa unashikiliwa na Majeshi ya Serikali.

Mji wa Khan Al Assal unatajwa ni moja ya maeneo yanayosemekana yameshuhudia matumizi ya silaha za kemikali na hivyo kutwaliwa na upinzani kunaweza kuchangia pakubwa kupoteza ushahidi huo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.