Pata taarifa kuu
AFRIKA KUSINI

Serikali ya Afrika Kusini yasema hali ya kiafya ya Nelson Mandela bado haijaimarika

Serikali ya Afrika Kusini inasema kuwa hali ya kiafya ya rais wa zamani wa nchi hiyo  Nelson Mandela bado haijaimarika na bado ni mbaya lakini thabiti.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa kutoka kwa Ofisi ya rais Jacob Zuma imewataka wananchi wa taifa hilo kuendelea kumwombea Mandela na familia yake.

Mandela anayefahamika kwa jina maarufu kama Madiba  kwa siku ya nne leo anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali moja jijini Pretoria.

Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 94 ambaye anasumbuliwa na mapafu alikimbizwa hospitalini siku ya Jumamosi  juma lililopita na madaktari wake wanasema hali yake ni mbaya lakini yuko katika hali thabiti.

Siku ya Jumapili Wakiristo nchini humo walifurika makanisani kumwombea Mandela ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la mapafu kwa kipindi kirefu.

Hii ni  mara ya nne kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita kwa Mandela ambaye atatimiza miaka 95 mwezi ujao kulazwa hospitalini na mara ya mwisho ilikuwa mwezi Aprili mwaka huu.

Mandela anakumbukwa sana kutokana na  mchango wake  mkubwa wa mapambano dhidi ya ya ubaguzi wa rangi nchini humo na kuwa rais wa kwanza mweusi mwaka 1994 baada ya kufungwa jela miaka 27 wakati wa  harakati za ukombozi.

Mara ya mwisho kwa Mandela kuonekana hadharini ilikuwa mwezi Julai mwaka 2010 wakati wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya kombe la dunia nchini humo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.