Pata taarifa kuu
BANGLADESH

Waumini wa Kiislam 32 wapoteza maisha kwenye maandamano nchini Bangladesh wakishinikiza kupitishwa kwa Sheria ya Kukufuru

Watu wapatao thelathini na wawili wamepoteza maisha nchini Bangladesh wakati jeshi la Polisi linazima maandamano ya Waumini wa Kiislam ambao walijitokeza kwenye Jiji la Kibiashara la Dhaka kushinikiza kupitishwa kwa sheria mpya ya kukufuru nchini humo.

Polisi nchini Bangladesh wakiwasambaratisha waumini wa kiislam wanaotaka kupitishwa kwa sheria mpya ya kukufuru
Polisi nchini Bangladesh wakiwasambaratisha waumini wa kiislam wanaotaka kupitishwa kwa sheria mpya ya kukufuru MUNIR UZ ZAMAN / AFP
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Bangladesh pia imechukua uamuzi wa kufunga Kituo Cha Televisheni cha Kiislam ambacho kinatajwa kuchochea kwa kiasi kikubwa kuzuka kwa maandamano hayo ya nchi nzima na kuchangia kuzuka ghasia wakati Polisi wakiwasambaratisha waandamaji.

Shughuli katika Jiji la Dhaka ambalo ndilo jiji kuu la kibiashara zimekwama kutokana na ghasia hizo zilizochochewa na Waumini wa Kiislam kudai sheria mpya ya kukufuru kutokana na ile iliyopo sasa kutokuwa na makucha kwa wale ambao hawaamini Dini ya Kiislam.

Waumini hao walipiga kambi Jijini Dhaka huku wakipaza sauti zao wakisema Mungu Mkubwa! Mungu Mkubwa! Na kusisitiza mtu atakayekutwa na hatia ya kukufuru inapaswa anyongwe badala ya ilivyo sasa.

Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi, madurugedi na kutoa sauti pamoja na maji ya kuwasha kuwasambatarisha zaidi ya waumini wa Kiislam wapatao elfu sabini waliopiga kambi katika Jiji la Dhaka wakitaka sheria hiyo ili kuwadhibiti wale wanoakufuru.

Msemaji wa Jeshi la Polisi katika Jiji la Dhaka Masudur Rahman amethibitisha jeshi hilo kutumia nguvu kuwasambaratisha waumini hao ambao wanatajwa walitumia mawe, fimbo za mianzi na matofali kuwashambulia askari waliokuwa wanawazuia kuendelea na maandamano.

Rahman amesema walialzima kufanya hivyo baada ya Jeshi la Polisi kuchoshwa na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vilikuwa vinafanywa na waumini hao waliokuwa wamepiga kambi kuonesha hasira zao juu ya kupitishwa kwa sheria hiyo mpya.

Naye Inspekta wa Polisi katika Jiji la Dhaka Mozammel Haq akiwa katika Hospital ya Chuo cha Dhaka amewaambia wanahabari wameshapokea miili ya watu kumi na moja waliopoteza maisha kutokana na kupigwa risasi pamoja na askari waliojeruhiwa.

Miili ya watu wengine kumi na moja imepelekwa kwenye Hospital nyingine za karibu huku waumini wengi ambao wamejeruhiwa wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospital tofauti katika Jiji la Dhaka.

Duru za kitabibu kutoka Hospital mbalimbali zinasema zaidi ya watu mia moja wamejeruhiwa kwenye ghasia hizo wengi wao vibaya na wanaendelea kupatiwa huduma ili warejee kwenye hali yao ya kawaida.

Ghasia hizo zilizuka mchana wa jumapili na kurindima kwa usiku kucha hadi hali iliporejea kama ilivyokuwa awali mapema asubuhi ya leo ambapo waumini hao walikuwa wanataka uwepo wa sheria mpya ya kukufuru na atakayekutwa na hatia anyongwe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.