Pata taarifa kuu
DRCONGO-RWANDA-HAGUE

Mahakama ya Kimataifa ICC yataka Ntaganda kufikishwa Hague haraka

Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imetaka kusafirishwa haraka kwa Bosco Ntaganda hadi katika Mahakama hiyo baada ya kujisalimisha katika Ubalozi wa Marekani nchini Rwanda siku ya Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Ofisi ya kiongozi wa Mashtaka mjini Hague imesema kuwa inawasiliana na serikali ya Rwanda pamoja na Marekani kuhakikisha kuwa Ntaganda anafika Hague ili kufunguliwa mashtaka yanayomkabili.

Mahakama hiyo ya ICC imeongeza kuwa kujisalimisha kwa Ntaganda ni habari njema kwa raia wote wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wameteseka mikononi mwa kiongozi huyo wa kundi la waasi.

Awali serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilipongeza hatua ya kujisalimisha kwa Jenerasli Bosco Ntaganda na kuomba Rwanda  kushirikiana na Mahakama ya ICC kumkabidhi kiongozi huyo katika Mahakama hiyo huko Hague.

Rwanda na Marekani ni kati ya mataifa ambayo hayajatia saini mkataba wa Kimataifa wa ICC lakini imekuwa ikishirikiana na Mahakama hiyo.

Kwa upande wake, msemaji wa mahakama ya ICC Fadi El Abdalah anasema kuwa Ntaganda anashtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita ikiwemo kuwasajili watoto kwenye jeshi lake, ubakaji, uporaji na unyanyasaji wa raia wakati akiwa kiongozi wa kundi la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa hatua hiyo ya Ntaganda kujisalimisha ni kubwa kwa harakati za kumaliza uasi Mashariki mwa nchi hiyo na mwanzo wa suluhu la amani kupatikana.

Naibu mwenyekiti na msemamji wa Mashirika ya kiraia Mashariki wa DRC, Omar Kavota ameimbia RFI Kiswahili kuwa kujisalimisha kwa Ntaganda ni ishara tosha kuwa viongozi wengine wa uasi Mashariki mwa nchi hiyo siku yao itafika ambapo hawatakuwa na lingine bali kujisalimsiha katika Mahakama hiyo ya ICC na kufunguliwa Mashtaka.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kuliripotiwa kuwa Ntaganda na viongozi wengine wa kundi la M 23 akiwemo Askofu Jean Marie Runinga walikimbilia Rwanda baada ya mapigano makali kuzuka kati ya kundi la M 23 linaloongozwa na Betrand Bissimwa na lile na Runiga.

Rwanda imekuwa ikituhumiwa na Umoja wa Mataifa kuwa inawaunga mkono waasi hao wa M 23 kwa kuwapa silaha madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.