Pata taarifa kuu
VATICAN

Papa Benedicto wa 16 aonekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kutangaza kujiuzulu

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Benedicto wa 16 ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu alipotangaza kuwa atajiuzulu wadhifa huo tarehe 28 mwezi huu wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na maelfu ya waumini wa Kanisa hilo katika makao Makuu ya Mtakatifu Petro Basilica mjini Vatican wakati akiongoza ibada ya kila wiki, Papa amewashukuru waumini wa Kanisa hilo na watu wengine duniani kwa kumwonesha upendo huku akiwarahi waendelee kumwombea kwa Mungu.

Akishangiliwa na maelfu ya watu wakati alipoanza kuzungumza ,kiongozi huyo amesema aliamua kujiuzulu kwa sababu ya Kanisa baada ya kuanza kupungua kwa nguvu za kuendelea kuongoza Kanisa hilo.

Hata hivyo, Vatican imesema Papa Benedicto wa 16 mwenye umri wa miaka 85 ataendelea na majukumu yake kama kawaida hadi mwisho wa mwezi huu atakapojiuzulu rasmi.

Kiongozi huyu wa Kanisa Katoliki atakumbukwa sana katika siku zijazo kwa kuwa Papa wa kwanza katika miaka ya hivi karibuni kutangaza kujiuzulu kinyume na wengine ambao wamekuwa wakifia uongozini.

Kiongozi huyo alichaguliwa kama Papa mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 78 na kuwa kiongozi wa Kanisa hilo akiwa na umri mkubwa zaidi katika historia ya kanisa hilo.

Kiongozi huyo alizaliwa nchini Ujerumani mwaka 1927 na jina lake halisi ni Joseph Ratzinger, na amekuwa akiliongoza Kanisa Katoliki kwa mwaka wa nane sasa baada ya kifo cha John Paul wa pili mwaka 2005.

Makadinali kutoka kote wanatarajiwa kukutana mjini Vatican mwezi ujao kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa hilo huku wachambuzi wa mambo wakisema huu ndio wakati wa Kanisa hilo kupata kiongozi nje ya bara la Ulaya.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.