Pata taarifa kuu
DRC-UGANDA

Kundi la M23 latishia kujitoa kwenye mazungumzo na serikali kama haitosaini makubaliano ya kusitisha mapigano

Kundi la Waasi la M23 ambalo linapambana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC limetishia kujiondoa kwenye mazungumzo ya kusaka suluhu ya mgogoro ambao unaendelea Mashariki mwa Taifa hilo iwapo serikali itashindwa kusaini makubaliano ya kuweka silaha chini. Waasi wa M23 wamemtaka Rais Joseph Kabila wa Kabange kusaini makubaliano hayo ili ujumbe wao urejee kwenye meza ya mazungumzo ambayo yanatarajiwa kuanza hii leo nchini Uganda baada ya kusitisha kwa majuma mawili kupisha sherehe za mwishoni mwa mwaka.

Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la Waasi la M23 Jean-Marie Runiga akishuka kwenye gari tayari kwa kuzungumza na waandishi wa habari huko Bunagana
Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la Waasi la M23 Jean-Marie Runiga akishuka kwenye gari tayari kwa kuzungumza na waandishi wa habari huko Bunagana Reuters/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la Waasi la M23 Jean-Marie Runiga Lugerero ndiye ametangaza msimamo wao wa huenda wakajitoa kwenye mazungumzo ya huko Kampala kama serikali haitasaini makubaliano na Kundi hilo ya kusitisha mapigano katika eneo la Mashariki.

Runiga amewaambia wanahabari kwenye mkutano wake ambao umefanyika eneo la Bunagana kwenye mpaka wa DRC na Uganda watakuwa tayari kupeleka ujumbe wao kampala iwapo serikali itakubaliana na pendekezo lao kinyume na hapo hawatoshiriki.

Kiongozi huyo wa M23 akizungumza kwa kujiamini amesema serikali ya Kinshasa ndiyo inayokwamisha mazungumzo hayo kuweza kufikia muafaka kutokana na kutokuwa tayari kusaini makuabaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Runiga amekiri kundi lake lina nia ya dhati ya kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanikiwa lakini serikali ndiyo kikwazo kwa sasa na kama iataendelea na msimamo wao ni wazi wanaweza wakauchukua tena Mji wa Goma kama walivyofanya mwezi Novemba.

Msemaji wa Serikali ya Kinshasa Lambert Mende ametupilia mbali madai ya Kundi la Waasi la M23 huku akisema wamekosa hoja za msingi na badala yake wameanza kutafuta sababu za kujiondoa kwenye mazungumzo hayo.

Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Kinshasa na Kundi la M23 kurejea mezani kwa mazungumzo baada ya mazungumzo ya awali yaliyoandaliwa huko Kampala kugonga mwamba kutokana na kila upande kung'ang'ania agenda zao.

Kundi la M23 linaongozwa na Bosco Ntaganda ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC limekuwa kitisha cha usalama katika eneo la Mashariki mwa DRC na kusababisha watu 800,000 kuyakimbia makazi yao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.