Pata taarifa kuu
LIBYA

Wabunge nchini Libya wamchagua Mohammed Magarief aliyekuwa mpinzani wa utawala ulioangushwa kuwa rais

Bunge nchini Libya limemchagua Mohammed Magarief kuwa Rais akitoka Chama Cha NFP ambacho kilipata wingi wa wabunge kwenye uchaguzi wa kwanza kufanyika kidemokrasia nchini humo baada ya kungushwa kwa Marehemu Kanali Muammar Gaddafi. 

Wabunge wa Libya wakimpongeza Mohammed Magarief baada ya kushinda uchaguzi na kuteuliwa kuwa rais
Wabunge wa Libya wakimpongeza Mohammed Magarief baada ya kushinda uchaguzi na kuteuliwa kuwa rais Reuters
Matangazo ya kibiashara

Magarief amemshinda Ali Zidan ambaye alikuwa anawania nafasi hiyo ambapo mshindi alipata kura mia moja na kumi na tatu huku mpinzani wake akiambulia kura themanini na tano kwenye uchaguzi uliofanyika kwa duru mbili.

Bunge lenye wabunge mia mbili limechagua rais huyo ambaye atamtaja Waziri Mkuu na kuliongoza bunge kwenye mchakato kupatikana kwa katiba ambayo itatoa nafasi ya kuitishwa kwa uchaguzi mkuu.

Ushindi wa kiongozi huyo ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala ulioangushwa kumeelezwa na wachambuzi wa mambo kuwa atachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko nchini humo kutokana na kuwa na msimamo wa kati.

Ushindi wa Magarief umeonekana kupokelewa kwa shangwe kubwa na wabunge wenzake pamoja na wananchi ambao moja kwa moja wameonesha kuwa na imani nae katika kuelekea kupata serikali mpya.

Kinachosubiriwa na wengi hivi sasa nchini Libya ni kuona serikali mpya inatangazwa na kwamba nani atapewa nafasi ya uwaziri mkuu kuongoza serikali mpya ya Libya.

Jumatano ya juma hili kiongozi wa baraza la mpito nchini humo lililoongoza mapinduzi kuung'oa utawala wa marehemu kanali Gaddafi ulikabidhi madaraka yake rasmi kwa bunge la nchi hiyo kama lilivyoahidi, hatua ambayo ilipokelewa kwa nderemo na wananchi wa Libya.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.