Pata taarifa kuu
Syria-Machafuko

Kofi Annan aomba Umoja wa Mataifa kuharakisha mchakato wa kuongezwa waangalizi wa Kimataifa nchini Syria

Msuluhishi wa kimataifa katika mgogoro wa Syria Kofi Annan amelitaka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kuharakisha mchakato wa kuongezwa kwa waangalizi wa Umoja huo zaidi ya 300 kwenda nchini Syria kusimamia zoezi la kusaka amani nchini humo wakati machafuko yakiendelea licha ya uwepo wa kundi la waangalizi nchini humo.

Kofi Annan, mpatanishi katika mgogoro wa Syria
Kofi Annan, mpatanishi katika mgogoro wa Syria REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Annan ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa baraza hilo na kueleza kuwa mashambulizi yanayoshuhudiwa sasa hayakubaliki hata kidogo na kukiri kuwa pande zote mbili zimeendelea kukiuka makubaliano ya awali ya kusitisha vita.

Annan ametaka waangalizi hao kutumwa nchini Syria ndani ya mwezi mmoja ujao. Msuluhishi huyo amesema kusikitishwa na hatuwa ya serikali ya rais Assad ya kupelekea vikosi vyake katika jiji la Hama, na kuwauwa watu zaidi ya thalathini siku ya jumatatu.

waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amesema kutiwa wasiwasi ha hali inayoendelea nchini Syria ambapo watu wanauawa baada ya kutowa ushahidi kwa waangalizi wa kimataifa, na kusema kuwa hatuwa hii inavuruga juhudi za kusaka amani katika nchi hiyo.

Waangalizi wa kimataifa wapo nchini Syria tangu April 16 mwaka huu na wanajaribu kutembelea miji mbalimbali ilioguswa zaidi na mashambulizi ya vikosi vya serikali ya rais Bashar Al Assad huku wakiandaa ujio wa waangalizi mia tatu kutoka Umoja wa Mataifa UN wanaotarajiwa kuanza kuwasili nchini humo mwanzoni mwa juma lijalo.

Upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameendelea kuitaka serikali ya Syria kuheshimu mapendekezo ya Annan na kutaka waangalizi wake kupatiwa ulinzi wa kutosha.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi mshirika wa karibu wa serikali ya rais Assad, Sergei Lavrov amewatahadharisha bila kuwataja, wale wote ambao amesema wanataka kuharibu malengo ya waangalizi wa Umoja wa Kimataifa UN nchini Syria

Katika hatua nyingine serikali ya rais Bashar Al-Assad imesema kuwa haitakubali waangalizi wowote toka umoja wa nchi za kiarabu na nchi za magharibi zinazojiita marafiki wa Syria.

Machafuko nchini Syria, yamesababisha vifo vya watu elfu kumi na moja na mia moja katika kipindi cha miezi kumi na tatu, kwa mujibu wa shirika linalo tetea haki za binadamu nchini Syria OSDH.

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.