Pata taarifa kuu
LIBYA-MAREKANI

Baraza la Mpito la Waasi Nchini Libya NTC lafungua ofisi ya Balozi nchini Marekani

Baraza la Mpito la Waasi Nchini Libya NTC hatimaye limefungua rasmi ofisi yake ya Ubalozi nchini Marekani kufuatia serikali ya Washington kulitambua kama utawala halali kipindi hiki ambacho juhudi zinashika kasi za kutaka kuangusha Utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.

Majeshi ya Waasi nchini Libya wakiendelea kutamba baada ya kumiliki eneo la Zawiyah
Majeshi ya Waasi nchini Libya wakiendelea kutamba baada ya kumiliki eneo la Zawiyah Reuters/Bob Strong
Matangazo ya kibiashara

Balozi Mpya wa NTC Ali Aujali amewasili Washington wakati huu ambapo serikali ya Marekani ikiwa kwenye mpango wa kutaka kuwapa mali na fedha walizokuwa wanazizuia kutoka kwa serikali ya Kanali Gaddafi.

Balozi Aujali baada ya kuwasili kwenye ofisi hiyo mpya akalakiwa na mamia ya wafuasi wa NTC na hapo ndipo akasema mara zote ofisi hiyo katika kipindi cha miaka arobaini na mbili imekuwa ikiwakilisha wananchi huru wa Libya.

Balozi huyo amesema Libya imezaliwa upya na ana matumaini watafanikiwa katika mpango wao ya kuuangusha Utawala wa Kanali Gaddafi na hivyo kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa kama nchi huru yenye demokarasia.

Aujali awali alikuwa ni Balozi wa Libya nchini marekani kabla ya kuasi serikali ya Kanali Gaddafi na kujiunga na Waasi wanaoungwa mkono na Mataifa ya Magharibi kwa kutumia Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.

Hatua ya NTC kufungua ofisi hiyo mpya inakuja baada ya majuma mawili serikali ya Marekani kupora ofisi hiyo kutoka kwa serikali ya Kanali Gaddafi ambayo wenyewe wanahubiri imepoteza uhalali wa kutawala.

Wakati huko nchini Marekani Waasi wakifungua ofisi yao ya Ubalozi nchini Libya mapambano makali yameendelea huku eneo la Zawayah likiendelea kuwa chini ya himaya ya NTC ambao wanahaha kuingia Tripoli.

Upande wa Serikali ya Kanali Gaddafi yenyewe imesema mji huo bado upo chini yao na kukanusha taarifa za Waasi kuwa wameyarudisha nyuma majeshi ya serikali kwa sasa.

Mapambano ya kutaka kuuangusha Utawala wa Kanali Gaddafi yamedumu kwa miezi sita sasa yakisaidiwa na Majeshi ya NATO ambayo yanatajwa kushambulia wananchi wasio na hatia na kuchangia vifo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.