Pata taarifa kuu
CAIRO-MISRI

Zaidi ya waandamanaji 500 wamejeruhiwa nchini Misri

Watu zaidi ya 590 wamejeruhiwa nchini Misri kufuatia mapambano yanayoendelea baina ya polisi na waandamaji katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo.

Mmoja wa waandamanaji nchini Misri akiwa na bendera ya nchi hiyo
Mmoja wa waandamanaji nchini Misri akiwa na bendera ya nchi hiyo Reuters
Matangazo ya kibiashara

Eneo la uwanja wa Tahrir ni maarufu sana nchini humo kwani ndilo eneo ambalo waandamanji hao walilitumia kufanya mkusanyiko uliopelekea kuangushwa kwa utawala wa rais Hosni Mubarak.

Maandamano hayo mapya ambayo bado chanzo chake hakijafahamika yanakuja ikiwa imepita miezi michache tangu kushuhudia watu zaidi ya mia moja wakipoteza maisha wakati wa harakati za kuuangusha utawala wa Mubarak.

Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo, imeeleza kusikitishwa kwake na maandamano hayo ambayo imeyaita ni haramu na hayana msingi wowote kwakuwa waandamanaji hawaelezi bayana kile wanachokitaka.

Polisi usiku wa jumanne walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji hao ambao walikuwa wanalenga kuvamia ofisi za kituo cha televisheni cha taifa cha nchi hiyo.

Baadhi ya waandamanaji waliohojiwa na vituo vya kimataifa wamesema kuwa maandamano hayo yanalenga kushinikiza serikali ya mpito kuharakisha kesi za waliokuwa mawaziri wa zamani wakati wa utawala wa Mubarak na kulipwa fidia kwa ndugu waliopoteza ndugu zao wakati wa maandamano ya mwezi wa kwanza mwaka huu.

Waziri mkuu wa Misri Essam Sharaf, tayari ameviagiza vikosi vya polisi kuondoka katika eneo la Tahrir hatua inayolenga kuleta hali ya amani katika eneo hilo dhidi ya waandamanaji hao.

Kiongozi huyo amewataka wananchi kuondoka kwa hiari katika uwanja huo, na kuwa wapeleke malalamiko yao kwa serikali ili yaweze kufanyiwa kazi.

Tangu kupinduliwa kwa rais wa zamani Hosni Mubarak na wananchi nchini humo mapema mwaka huu maandamano yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kushinikiza mabadiliko zaidi katika serikali ya kijeshi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.