Pata taarifa kuu
THE HEAGUE

Majaji wa mahakama ICC watoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi

Majaji wa mahakama ya kimataifa inayoshughulikia wahalifu wa kivita ya ICC wametoa hati rasmi ya kimataifa ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya kanali Muamar Gaddafi pamoja na mtoto wake Seif al-Islam na aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa Abdullah al-Senussi.

Kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi
Kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi Wikipedia/profile
Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa majaji watakaosikiliza kesi hiyo Sanji Mmasenono Monageng ndie aliyetangaza uamuzi wa mahakama hiyo muda mfupi uliopita na kusema kuwa wameridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakam hiyo Luis Moreno Ocampo dhidi ya kiongozi huyo na washirika wake.

“Napenda kutangaza ya kwamba, hii leo jopo la majaji wa mahakama hii, kwa kauli moja limeridhia ushahidi uliowasilihswa na mwendesha mashataka na hivyo tunatangaza rasmi kutoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa kanali Moamer Gaddafi na washirika wake”.

Washukiwa wote watatu wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita ikiwemo vitendo vya ubakaji, ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na kuamuru kuuawa kwa wananchi wasio na hatia.

Kutolewa kwa hati hiyo ya kimataifa kunakuja wakati ambapo bado kiongozi huyo wa Libya ameendelea kusalia madarakani huku kukiwa hakuna dalili ya lini ataondoka madarakani kupisha serikali ya mpito inayopigiwa chapuo na jumuiya ya kimataifa ukiwemo umoja wa Afrika AU.

Tayari baadhi ya nchi kama vile za Uingereza na Marekani zimepongeza uamuzi wa majaji wa mahakam hiyo kwa kutoa hati hiyo ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wakisema kuwa kutaharakisha upatikanaji wa haki nchini Libya.

Nao viongozi wa Umoja wa Afrika walioko nchini Libya kwa mazungumzo na serikali ya Libya pamoja na waasi wanaoipinga serikali wametoa taarifa wakisema kuwa kanali Gaddafi ametangaza kutoshiriki katika mazungumzo yoyote ya kutafuta amani na badala yake ni maofisa wake ndio watakaoshiriki.

Wakati huohuo maelfu ya wananchi wamejikusanya katika mji wa Misrata wakiwa na mabango yanayoutuhumu utawala wa Gaddafi huku nao pia wakisema watatoa ushahidi unaoonyesha kuhusika kwa vikosi vya kiongozi huyo dhidi ya mauaji ya raia.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema kuwa kutolewa kwa hati hiyo ya kimataifa ni ushindi kwa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya unyanysaji vinavyofanywa na vikosi vya Libya.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.