Pata taarifa kuu

Uvujaji wa nyaraka za siri Marekani: Askari mwenye umri wa miaka 21 afikishwa mahakamani

Kijana mwenye umri wa miaka 21, Jack Teixeira, anayeshukiwa kuwa chanzo cha mojawapo ya kashfa nzito za uvujaji wa nyaraka za siri kwa miaka kumi nchini Marekani, anatarajia kufikishwa mahakamani Ijumaa siku moja baada ya kukamatwa kwake.

Maafisa wa FBI wakimkamata Jack Teixeira (aliyevalia kaptula ya rangi nyekundu) huko North Dighton, Massachusetts (Marekani) mnamo Aprili 13, 2023.
Maafisa wa FBI wakimkamata Jack Teixeira (aliyevalia kaptula ya rangi nyekundu) huko North Dighton, Massachusetts (Marekani) mnamo Aprili 13, 2023. via REUTERS - WCVB-TV
Matangazo ya kibiashara

Jack Teixeira, 21, ni mmoja wa askari wa kikosi cha  walinzi wa taifa huko Massachusetts. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Ijumaa.

Mfanyakazi huyu mdogo wa kikosi cha walinzi wa kitaifa 'alikamatwa bila purukushani yoyote' Alhamisi huko Dighton, mji mdogo wa mashambani kusini mwa Boston, katika jimbo la Massachusetts (kaskazini mashariki), kulingana na Waziri wa Sheria Merrick Garland. Kukamatwa kwake kulitangazwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya Marekani.

Anashukiwa kuwa ameweka hatari kubwa kwa usalama wa taifa wa Marekani, kulingana na Pentagon, kwa kufichua nyaraka za siri mtandaoni kuhusu vita vya Ukraine na ambazo pia zinaonyesha kuwa Washington inakusanya taarifa za kijasusi kwa washirika wake muhimu wa karibu , ikiwa ni pamoja na Israel na Korea Kusini. Jambo la aibu zaidi kwa serikali ya Rais Joe Biden.

Kijana huyo anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya Massachusetts siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa chanzo cha Idara ya Haki.

Vituo vya televisheni vimerusha picha za angani siku ya Alhamisi zikionyesha kukamatwa kwake. Katika video hizi anaonekana mwanamume, akiwa ameweka mikono kichwani na aliyevalia fulana ya kijivu na kaptula nyekundu, akirudi taratibu kuelekea kwa maafisa wenye silaha kabla ya kukamatwa na kisha kusindikizwa kwenye gari.

Biden 'atiwa wasiwasi'

Joe Biden, anayezuru Ireland, amefahamishwa juu ya kukamatwa kwa kijana huyo, kulingana na Ikulu ya White House. "Nina wasiwasi kuwa hili limetokea," amesema mapema kuhusu nyaraka za siri zilizovuja ambazo Idara ya Sheria ya Marekani imefungua uchunguzi wa makosa ya jinai.

Gazeti la kila siku la Washington Post liliripoti Jumatano kwamba uvujaji huo ulikuwa kazi ya kijana mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya kijeshi, ambaye alishiriki taarifa zake kwenye kundi la kibinafsi la mtandaoni kwenye mtandao wa kijamii wa Discord. Chini ya jina la uwongo "OG", mshukiwa alikuwa amechapisha kwa miezi kadhaa hati kutoka kituo cha kijeshi anakofanya kazi.

Mlinzi wa Kitaifa alisema Jack Teixeira alijiandikisha mnamo Septemba 2019, alifanya kazi kama mtaalamu wa kompyuta na mawasiliano na akapata kiwango cha Daraja la Kwanza la Airman, cheo cha tatu kwa kuanzia chini katika uongozi.

"OG" alikuwa amewataka washiriki wengine wa kikundi cha Discord kutosambaza hati hizo, akihakikisha kwamba hakuwa na nia ya kuwa mtoa taarifa, kulingana na Gazeti la Washington Post. Alikuwa akiikosoa serikali - ambapo aliishtumu kwa "matumizi mabaya ya mamlaka" -, pia alikuwa akiikooa polisi na mashirika ya kijasusi  ya Marekani.

Kundi hilo, linaloundwa na watu wapatao 24, baadhi yao wakitoka Urusi na Ukraine, lilianzishwa mwaka 2020 kwa ushirikiano wao wa karibu kuhusiana na masuala ya silaha, zana za kijeshi na dini. Jack Teixeira alikuwa kiongozi wa kundi hilo, Gazeti la  New York Times limeripoti.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre alisema Marekani inachunguza "madhara" ya uvujaji huo "kwa usalama wa taifa". Pentagon pia imeamua kuzuia zaidi ufikiaji wa aina hii ya habari nyeti, Jean-Pierre amewaambia waandishi wa habari.

Msemaji huyo aliongeza kuwa serikali ya Marekani inataka mitandao ya kijamii "kuepusha kuwezesha" usambazaji wa nyaraka hizo za siri, ikiamini kuwa zina "wajibu kwa watumiaji wake na kwa nchi".

Msemaji wa Discord aliiambia AFP kwamba usalama wa watumiaji wake ndio kipaumbele cha jukwaa, kuhakikisha kwamba inashirikiana na utekelezaji wa sheria.

Ukweli kwamba hati hizi kusambazwa mtandaoni inawakilisha "hatari kubwa sana kwa usalama wa taifa na ina uwezo wa kuchochea taarifa potofu", alisema Jumatatu msemaji wa Idara ya Ulinzi ya Marekani, Chris Meagher.

Nyaraka zilizochapishwa mtandaoni zinaonyesha hasa wasiwasi wa idara za kijasusi za Marekani kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya Ukraine dhidi ya vikosi vya Urusi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.