Pata taarifa kuu

CAR: Kiongozi wa upinzani ahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela

Kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Crépin Mboli Goumba, amehukumiwa siku ya Jumatano kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kukashifu na kudharau mahakama, katika nchi ambayo sauti ya upinzani au ukosoaji inakandamizwa na mamlaka ya rais Faustin Archange Touadéra.

Crepin Mboli-Goumba (Katikati) akiwasili Bangui Januari 15, 2013.
Crepin Mboli-Goumba (Katikati) akiwasili Bangui Januari 15, 2013. © PATRICK FORT / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wakili huyu, mratibu wa jukwaa kuu la upinzani, Kambi ya Jamhuri inayotetea Katiba (BRDC), alikuwa amewashtaki baadhi ya mahakimu kula njama na washtakiwa au hata kuwa wafisadi, na kukosoa kwamba "haki haitendeki tena kwa niaba ya raia.”

Alikamatwa mnamo Machi 3 na kuwekwa kizuizini kwa siku tatu. Mahakama ya mwanzo ya Bangui ilimhukumu siku ya Jumatano kifungo cha mwaka mmoja jela na kulipa faini ya faranga milioni 80 za CFA (karibu euro 122,000) kama fidia iliyogawanywa kati ya majaji wanne ambao aliwashutumu kwa "kuwatusi" na "kuwachafua", kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP.  aliyehudhuria kesi hiyo.

Bw. Mboli Goumba ameondoka mahakamani akiwa huru na mawakili wake ambao wamelaani kesi ya “kisiasa” wakibaini kwamba watakata rufaa. Upinzani, ambao mikutano na maandamano yao yanakaribia kupigwa marufuku, mara kwa mara yanakabiliwa na vitisho nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa yanashutumu mara kwa mara.

Mbunge wa upinzani, Dominique Yandocka, anafungwa tangu Desemba 15, licha ya kinga yake ya ubunge, kwa "jaribio la mapinduzi" ambalo upande wa mashtaka bado haujathibitisha hadharani.

Utawala wa Bw. Touadéra "unakandamiza mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na vyama vya siasa vya upinzani", liliandika shirika la Human Rights Watch (HRW) mwezi Aprili 2023, likitaja "wasiwasi mkubwa kuhusu hatari katika suala la ukiukwaji wa haki za binadamu na kupunguzwa kwa nafasi ya kidemokrasia na uhuru wa kujieleza.

HRW pia iliitaka serikali ya Bw. Touadéra "kuhakikisha uhuru wa mahakama ili kuhakikisha kwamba wale waliohusika wanaoshambulia wakosoaji wa serikali wanachukuliwa hatua." Bw. Touadéra alibadilisha Katiba mnamo mwezi wa Julai 2023 na kura ya maoni iliyosusiwa na upinzani, ili kujiidhinisha kugombea muhula wa tatu mwaka wa 2025.

Alichaguliwa mwaka 2016 katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, alichaguliwa tena mwaka 2020 chini ya masharti yaliyopingwa na upinzani na katika nchi ambayo sehemu kubwa ya eneo hilo ilikuwa inadhibitiwa na waasi, ambao jeshi lake liliwarudisha nyuma kwa msaada wa Moscow na uingiliaji mkubwa wa mamluki wa Wagner kutoka Urusi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.