Pata taarifa kuu

Sudan Kusini: Watu 18 wauawa wakiwemo wanajeshi 8 katika mapigano

Watu 18, wakiwemo wanajeshi wanane, waliuawa katika mashambulizi ya kundi lenye silaha magharibi mwa Sudan Kusini siku ya Jumatatu, kaimu gavana wa jimbo hilo ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumanne.

Mapigano hutokea mara kwa mara katika jimbo la Abyei, ambalo hali yake haijatatuliwa tangu uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011.
Mapigano hutokea mara kwa mara katika jimbo la Abyei, ambalo hali yake haijatatuliwa tangu uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011. © AFP
Matangazo ya kibiashara

 

"Wanane ni wanajeshi na kumi ni raia. Ilikuwa asubuhi (ya Jumatatu) ambapo washambuliaji walishambulia kituo cha polisi" huko Tharkueng Payam, kaimu gavana wa jimbo la Bahr el Ghazal Magharibi, Arkenjelo Anyar Anyar ameliambia shirika la habari la AFP. Miongoni mwa raia waliouawa, "ni watoto, wanawake, wazee. Walichomwa moto kwa sababu hawakuweza kukimbia," gavana amebaini. Ameongeza kuwa zaidi ya watu 2,000 wamekimbia makazi yao.

Kulingana na Arkenjelo Anyar Anyar, "vijana wenye silaha" kutoka jimbo jirani la Warrap walichoma moto soko, nyumba na kituo cha polisi kutokana na mzozo wa ardhi. "Hali sasa imedhibitiwa," naibu gavana amesema.

Siku ya Jumatano, takriban watu 39 waliuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika mapigano kati ya makundi mawili ya wafugaji kutoka majimbo jirani katikati mwa nchi. Kati ya mwisho wa mwezi wa Januari na mwanzoni mwa mwezi wa Februari, takriban watu 73 waliuawa katika mashambulizi ya kikabila kati ya Ngok na Twic, matawi mawili ya kabila la Dinka, ambalo ni kubwa zaidi nchini, katika mkoa wa Abyei, eneo la mpaka linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Mapigano hutokea mara kwa mara huko Abyei, ambayo hadhi yake haijatatuliwa tangu uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011 na ambayo iko chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa. Siku ya Jumanne, Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar walitoa wito kwenye mtandao wa X "kukomesha ghasia", wakielekeza hasa "mgogoro wa ardhi kati ya jamii za Ngok na Twic".

Migogoro hii inakuja kujiongeza kwenye ghasia za kisiasa za kikabila ambazo zinadhoofisha nchi hiyo changa zaidi duniani, ambayo ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011. Sudan Kusini ilmetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya viongozi hasimu Riek Machar na Salva Kiir, ambavyo vimegharimu maisha ya watu karibu 400,000 na mamilioni kuhama makazi yao kati ya mwaka 2013 na 2018.

Mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka wa 2018 unatoa kanuni ya kugawana mamlaka ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa, Bw. Kiir akiwa rais na Bw. Machar kama makamu wa rais. Lakini kwa kiasi kikubwa imesalia kutotekelezwa, kutokana na mizozo inayoendelea kati ya mahasimu hao wawili, na kuifanya nchi hiyo kukumbwa na ghasia, ukosefu wa utulivu na umaskini, licha ya rasilimali zake za mafuta.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.