Pata taarifa kuu

DRC: Askofu Mkuu wa Kinshasa aelezea uchaguzi kama 'machafuko makubwa'

Katika misa yake ya Krismasi, Askofu Mkuu wa Kinshasa ameelezea Jumapili jioni uchaguzi wa wiki hii nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama "machafuko makubwa yaliyopangwa", wakati tume ya uchaguzi ikiendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa rais.

Kadinali Fridolin Ambongo Besungu, wakati wa Misa ya Krismasi kwenye Kanisa Kuu la Notre-Dame du Kongo mjini Kinshasa, Desemba 24, 2023.
Kadinali Fridolin Ambongo Besungu, wakati wa Misa ya Krismasi kwenye Kanisa Kuu la Notre-Dame du Kongo mjini Kinshasa, Desemba 24, 2023. © PATRICK MEINHARDT / AFP
Matangazo ya kibiashara

Kanisa Katoliki lina ushawishi mkubwa na kijadi linakosoa mamlaka nchini DRC.

"Kwa shauku, kwa dhamira, wengi wetu tulijitokeza kueleza mapendeleo yetu kidemokrasia," ametangaza Kardinali Fridolin Ambongo mbele ya waumini waliokusanyika katika kanisa kuu la Notre-Dame du Kongo, katika wilaya ya Gombe huko Kinshasa.

"Lakini ole," ameongeza, "kile ambacho kingekuwa sherehe kubwa ya maadili ya kidemokrasia kiligeuka kuwa mfadhaiko kwa wengi."

Uchaguzi ulikuwa "machafuko makubwa yaliyopangwa. Nyote ni mashahidi wa hilo", alisema askofu mkuu, ambaye alitaja "picha zisizoweza kuvumilika", akizungumzia video inayoonyesha shambulio dhidi ya mwanamke aliyepigwa kikatili na kudhalilishwa kwa sababu alipigia kura upinzani.

"Tunatoa taswira gani ya nchi yetu duniani? Tunawezaje kuwa na tabia chafu zisizovumilika kama hizi?", amesema kasisi huyo, katika ujumbe wake alioutoa kwanza kwa Kifaransa, kisha kwa Lingala.

Takriban wapiga kura milioni 44, kati ya takriban wakazi milioni 100 wa DRC, nchi kubwa zaidi ya Kikatoliki barani Afrika, waliitwa kumchagua rais wao, wabunge wao wa kitaifa na mikoa na madiwani wao wa manispaa siku ya Jumatano.

Mkuu wa nchi anayemaliza muda wake, Félix Tshisekedi, anawania muhula wa pili dhidi ya wagombea wengine 18, ambao baadhi yao wameshutumu "machafuko" na "makosa" ambayo wanaamini yaliharibu uchaguzi. Baadhi wanapanga maandamano Jumatano ijayo, wengine wakitaka uchaguzi ufutiliwe mbali moja kwa moja.

Miongoni mwa wapinzani hao ni pamoja na Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa mkoa wenye madini wa Katanga (kusini-mashariki), Martin Fayulu, ambaye anadai ushindi uliibiwa kutoka kwake katika uchaguzi wa mwaa 2018, na Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa huduma yake aliyoitoa kwa waathiriwa wanawake waliobakwa wakati vita vilikuwa vikipamba moto nchini DRC.

Matokeo ya mikoa

Kutokana na matatizo mengi ya vifaa, muda wa kupiga kura uliongezwa na tume ya uchaguzi (CENI). Uchaguzi huo ulimalizika rasmi siku ya Alhamisi jioni lakini uliendelea hadi wikendi katika maeneo ya mbali ya mikoa kadhaa.

"Kwa sasa, ninawaomba muwe waangalifu na wenye kujizuia," Kardinali Ambongo alisema. Siku moja kabla, karibu balozi kumi na tano zilitoa wito huo.

"Tunasubiri ripoti kutoka kwa jumbe mbalimbali za waangalizi, hasa ile ya misheni ya pamoja ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiprotestanti, ambayo inaweza kutusaidia kutathmini dosari zilizojitokeza na kutathmini athari zake katika uaminifu wa chaguzi hizi". alibainisha.

Wakati huo huo na katika wilaya hiyo, kutoka kituo chake cha uendeshaji kilichoundwa mahsusi kwa ajili ya uchaguzi, CENI iliendelea kutangaza sehemu ya matokeo ya uchaguzi wa urais, shughuli iliyoanza siku ya Ijumaa pamoja na kura kutoka nchi za kigeni ambako raia wa DRC waliruhusiwa kupiga kura.

Matokeo yanayojumuisha takriban wapiga kura milioni moja, waliokusanywa katika maeneo 22 katika mikoa kadhaa, yalitolewa jioni. Takwimu hizi, ambazo bado si muhimu, zinamweka Félix Tshisekedi vizuri sana katika uongozi, akiwa na alama ya karibu 80%.

CENI inapanga kutoa matokeo mengine siku ya Jumatatu.

Kutangazwa kwa mshindi kunaweza kufuatiwa na machafuko, katika nchi hii yenye historia yenye misukosuko ya kisiasa na mara nyingi iliyokumbwa na vurugu, yenye ardhi yenye madini mengi lakini ambayo wakazi wake wengi ni maskini.

Mbali na tuhuma za wapinzani tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi, kampeni za uchaguzi zilitishiwa na hali ya usalama mashariki mwa DRC, ambayo imekuwa na kilele cha mvutano kwa miaka miwili na kuibuka tena kwa uasi wa M23, unaoungwa mkono na Rwanda, kulingana na ripoti mbalimbali za wataalamu wa Umoja wa Mataifa na serkali ya DRC.

Baadhi ya wagombea wa upinzani wameshutumiwa kuwa "raia wa kigeni", silaha kubwa ya kuwavunjia heshima katika nchi hii iliyokumbwa na mizozo ya miaka mingi.

Katika hali hii ya wasiwasi baada ya uchaguzi, tangazo la kifo cha mtaalamu wa Ubelgiji, aliyekuwepo Kinshasa kama sehemu ya ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Ulaya siku ya Jumapili asubuhi, lilizua tafsiri mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii. Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia, hakuna shaka kwamba mtu huyu aliuawa kwa kupewa sumu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.