Sudan: Marekani yatoa wito kwa RSF kuacha kushambulia maeneo ya raia
Marekani imewataka wapiganaji wa RSF nchini Sudan kuacha kushambulia kwa makombora maeneo ya makazi ya raia, Washington ikisema hatua hiyo inazidisha mateso kwa raia Sudan.
Imechapishwa:
Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imetoa wito kwa RSF kuhakikisha raia katika maeneo ya Nyala, Omdurman, na kote Sudan wanalindwa badala ya kuwashambulia.
Wapiganaji wa RSF na jeshi la Sudan wamekuwa wakipigana tangu Aprili katika mzozo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 5,000 na wengine zaidi ya milioni tano kukimbia makazi yao, kulingana na ripoti ya UN.
Katika siku za hivi majuzi RSF imeonekana kuongeza mashambulio kwenye maeneo yanayodhibitiwa na jeshi huko Omdurman, hatua ambayo imesababisha vifo vya raia.
Kundi hilo pia limeendelea kuzingira kambi za kijeshi huko Nyala magharibi mwa jimbo la Darfur kwa nia ya kuuteka mji huo.
Marekani pia imerejelea wito wake kwa RSF na jeshi la Sudan kusitisha mapigano mara moja na kuanza tena mazungumzo ya kumaliza mzozo huo.
Washington tayari imeweka vikwazo kwa makampuni yanayohusishwa na RSF na jeshi, pamoja na viongozi wawili wa RSF wanaotuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Mazungumzo ya amani yaliyoongozwa na Marekani na Saudi Arabia kati ya RSF na jeshi yalivunjika mwezi Julai.