Pata taarifa kuu

DRC: Familia mjini Bukavu zahofia mioto ya mara kwa mara

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo nyumba zaidi ya hamsini na maduka zaidi ya kumi yameteketea moto usiku wa kuamkia Alhamisi katika maeneo ya Panzi na Mudaka kwenye viunga vya mji wa Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini.  

Watu wakileta maji kuzima moto katika maduka yaliyoungua baada ya ajali ya DC-9 huko Goma Aprili 15, 2008.
Watu wakileta maji kuzima moto katika maduka yaliyoungua baada ya ajali ya DC-9 huko Goma Aprili 15, 2008. (Photo : AFP)
Matangazo ya kibiashara

Mashuhuda wanasema moto mkali umewaka Jumatano jioni na kuteketeza baadhi ya nyumba zilizojengwa kwa mbao katika eneo la Panzi/Mulungulungu, bila kufafanua zaidi chanzo cha moto huo.  

Moto mwingine umeteketeza maduka kadhaa kwenye soko la Mudaka, likiwa soko la pili kiuchumi katika wilaya ya Kabare linalopatikana kwenye umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa mji wa Bukavu ambapo pia raia wa Bukavu hununua bidhaa mbalimbali.  

Katika taarifa ya hivi karibuni, huduma ya ukingo wa raia Kivu kusini imehakikisha kwamba tangu Aprili mwaka huu tayari watu 18 wamepoteza maisha, watu wawili wamejeruhiwa na zaidi ya nyumba elfu moja kuteketea katika mfululizo wa ajali za moto zinazokadiriwa kuwa zaidi ya 20 mjini Bukavu.  

Alipotangaza takwimu hizo, Aimé Lubago ambaye ni kiongozi wa huduma hiyo kwenye ofisi ya meya wa Bukavu, amesema familia zaidi ya elfu mbili zimebaki bila makazi zikiwa pia na matatizo makubwa ya kiuchumi.  

Kiongozi huyo amenyoshea kidole ujenzi wa kiholela, kamba za moto wa umeme zilizotelekezwa kiholela na haswa zaidi mafuta ya gari yanayohifadhiwa na wauzaji wadogowadogo katika baadhi ya nyumba za Bukavu.  

Huduma ya zimamoto imeonya wakaazi wa Bukavu kuwa waangalifu, ikihakikisha kwamba mji huo una magari matatu pekee ya zimamoto ambayo hadi sasa, yana matatizo ya kiufundi ambayo yanatafutiwa suluhisho.  

Hivi karibuni Spika wa baraza la seneti nchini Congo Modeste Bahati Lukwebo amenunua magari tano ya zimamoto na kuyakabidhi viongozi wa mitaa ya Bukavu, ila wadadisi wa mambo wanahisi kwamba hadi sasa magari hayo hayajatumika kama ilivyotarajiwa, kukiwa pia na tatizo la ujenzi kiholela unaozuia magari ya zimamoto kufikia maeneo ya ajali ya moto.  

 

Ripoti yake mwandishi wa RFI Kiswahili huko Bukavu, William Basimike.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.